Ezekieli 28

Unabii Dhidi Ya Mfalme Wa Tiro

1 Neno laBwanalikanijia kusema:

2 “Mwanadamu, mwambie mfalme wa Tiro, ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo:

“ ‘Kwa sababu moyo wako umejivuna

na umesema, “Mimi ni mungu;

nami ninaketi katika kiti cha enzi cha mungu

katika moyo wa bahari.”

Lakini wewe ni mwanadamu, wala si mungu,

ingawa unafikiri kuwa una hekima kama mungu.

3 Je, wewe una hekima kuliko Danieli?

Je, hakuna siri iliyofichika kwako?

4 Kwa hekima yako na ufahamu wako,

umejipatia utajiri,

nawe umejikusanyia dhahabu

na fedha katika hazina zako.

5 Kwa werevu wako mwingi katika biashara,

umeongeza utajiri wako

na kwa sababu ya utajiri wako

moyo wako umekuwa na kiburi.

6 “ ‘Kwa hiyo, hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo:

“ ‘Kwa sababu unafikiri una hekima,

mwenye hekima kama mungu,

7 mimi nitawaleta wageni dhidi yako,

taifa katili kuliko yote;

watafuta panga zao dhidi ya uzuri wa hekima yako,

na kuchafua fahari yako inayong’aa.

8 Watakushusha chini shimoni,

nawe utakufa kifo cha kikatili

katika moyo wa bahari.

9 Je, wakati huo utasema, “Mimi ni mungu,”

mbele ya wale wanaokuua?

Utakuwa mwanadamu tu, wala si mungu,

mikononi mwa hao wanaokuua.

10 Utakufa kifo cha wasiotahiriwa

kwa mkono wa wageni.

Kwa kuwa mimi nimenena, asemaBwanaMwenyezi.’ ”

11 Neno laBwanalikanijia kusema:

12 “Mwanadamu, mfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, nawe umwambie: ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo:

“ ‘Ulikuwa kipeo cha ukamilifu,

ukiwa umejaa hekima

na mkamilifu katika uzuri.

13 Ulikuwa ndani ya Edeni,

bustani ya Mungu;

kila jiwe la thamani lilikupamba:

akiki nyekundu, yakuti manjano na zumaridi,

krisolitho, shohamu na yaspi,

yakuti samawi, almasi na zabarajadi.

Kuwekwa kwa hayo mapambo na kushikizwa kwake

kulifanywa kwa dhahabu;

siku ile ulipoumbwa yaliandaliwa tayari.

14 Ulitiwa mafuta kuwa kerubi mlinzi,

kwa kuwa hivyo ndivyo nilivyokusimika.

Ulikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu;

ulitembea katikati ya mawe ya moto.

15 Ulikuwa mnyofu katika njia zako

tangu siku ile ya kuumbwa kwako,

hadi uovu ulipoonekana ndani yako.

16 Kutokana na biashara yako iliyoenea,

ulijazwa na dhuluma

nawe ukatenda dhambi.

Hivyo nilikuondoa kwa aibu kutoka katika mlima wa Mungu,

nami nikakufukuza, Ee kerubi mlinzi,

kutoka katikati ya mawe ya moto.

17 Moyo wako ukawa na kiburi

kwa ajili ya uzuri wako,

nawe ukaiharibu hekima yako

kwa sababu ya fahari yako.

Kwa hiyo nikakutupa chini;

nimekufanya kioja mbele ya wafalme.

18 Kwa dhambi zako nyingi na biashara yako ya dhuluma,

umenajisi mahali pako patakatifu.

Kwa hiyo nilifanya moto utoke ndani yako,

nao ukakuteketeza,

nami nikakufanya majivu juu ya nchi,

machoni pa wote waliokuwa wakitazama.

19 Mataifa yote yaliyokujua

yanakustajabia;

umefikia mwisho wa kutisha

na hutakuwepo tena milele.’ ”

Unabii Dhidi Ya Sidoni

20 Neno laBwanalikanijia kusema:

21 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Sidoni, ukatabiri dhidi yake,

22 nawe useme: ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo:

“ ‘Mimi ni kinyume chako, Ee Sidoni,

nami nitapata utukufu ndani yako.

Nao watajua kwamba Mimi ndimiBwana,

nitakapotekeleza hukumu zangu

na kuonyesha utakatifu wangu ndani yake.

23 Nitapeleka tauni ndani yake

na kufanya damu itiririke katika barabara zake.

Waliochinjwa wataanguka ndani yake,

kwa upanga dhidi yake kila upande.

Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimiBwana.

24 “ ‘Nyumba ya Israeli hawatakuwa tena na majirani wenye nia ya kuwadhuru wanaoumiza kama michongoma na miiba mikali. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimiBwanaMwenyezi.

25 “ ‘Hili ndiloBwanaMwenyezi asemalo: Nitakapoikusanya nyumba ya Israeli kutoka katika mataifa ambako wametawanyika, nitajionyesha kuwa mtakatifu miongoni mwao machoni pa mataifa. Ndipo watakapoishi katika nchi yao wenyewe, niliyompa mtumishi wangu Yakobo.

26 Wataishi humo kwa salama na watajenga nyumba na kupanda mashamba ya mizabibu, wataishi kwa salama nitakapowaadhibu majirani zao wote ambao waliwafanyia uovu. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimiBwana, Mungu wao.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EZK/28-c103ccfad913a2740d4a2fb7d66b7a6b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × two =