Isaya 10

1 Ole wao wawekao sheria zisizo za haki,

kwa wale watoao amri za kuonea,

2 kuwanyima maskini haki zao

na kuzuilia haki za watu wangu walioonewa,

kuwafanya wajane mawindo yao

na kuwanyang’anya yatima.

3 Mtafanya nini siku ya kutoa hesabu,

wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali?

Mtamkimbilia nani awape msaada?

Mtaacha wapi mali zenu?

4 Hakutasalia kitu cho chote

isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka

au kuanguka miongoni mwa waliouawa.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

Hukumu Ya Mungu Juu Ya Ashuru

5 “Ole wa Waashuru, fimbo ya hasira yangu,

ambaye mkononi mwake

iko rungu ya ghadhabu yangu!

6 Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu,

ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha,

kukamata mateka na kunyakua nyara,

pia kuwakanyaga chini

kama matope ya barabarani.

7 Lakini hili silo analokusudia,

hili silo alilonalo akilini;

kusudi lake ni kuangamiza,

kuyakomesha mataifa mengi.

8 Maana asema, ‘Je, wafalme wote

si majemadari wangu?

9 Je, Kalno hakutenda kama Karkemishi?

Hamathi si kama Arpadi,

nayo Samaria si kama Dameski?

10 Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu,

falme ambazo vinyago vyao

vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria:

11 je, nisiishughulikie Yerusalemu na sanamu zake

kama nilivyoshughulikia

Samaria na vinyago vyake?’ ”

12 Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.”

13 Kwa kuwa anasema:

“ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili,

kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu.

Niliondoa mipaka ya mataifa,

niliteka nyara hazina zao,

kama yeye aliye shujaa

niliwatiisha wafalme wao.

14 Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota,

ndivyo mkono wangu

ulivyochukua utajiri wa mataifa;

kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa,

ndivyo nilivyokusanya nchi zote;

wala hakuna hata mmoja aliyepigapiga bawa

au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”

15 Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi

kuliko yule anayelitumia,

au msumeno kujisifu

dhidi ya yule anayeutumia?

Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye,

au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!

16 Kwa hiyo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

atatuma ugonjwa wa kudhoofisha

kwa askari wake walio hodari,

katika fahari yake moto utawaka

kama mwali wa moto.

17 Nuru ya Israeli itakuwa moto,

Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto;

katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba

na michongoma yake.

18 Fahari ya misitu yake

na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa,

kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.

19 Nayo miti inayobaki katika misitu yake

itakuwa michache sana

kwamba hata mtoto mdogo

angeweza kuihesabu.

Mabaki Ya Israeli

20 Katika siku ile mabaki ya Israeli,

walionusurika wa nyumba ya Yakobo,

hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga,

lakini watamtegemea kwa kweli

BwanaAliye Mtakatifu wa Israeli.

21 Mabaki watarudi, mabaki wa Yakobo

watamrudia Mungu Mwenye Nguvu.

22 Ingawa watu wako, Ee Israeli,

ni wengi kama mchanga kando ya bahari,

ni mabaki yao tu ndio watakaorudi.

Maangamizi yamekwisha amriwa,

ni mengi tena ni haki.

23 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

atatimiza maangamizi

yaliyoamriwa juu ya nchi yote.

24 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote asemalo:

“Enyi watu wangu mkaao Sayuni,

msiwaogope Waashuru,

wanaowapiga ninyi kwa fimbo

na kuinua rungu dhidi yenu,

kama Misri ilivyofanya.

25 Bado kitambo kidogo

sana hasira yangu dhidi yenu itakoma,

na ghadhabu yangu itaelekezwa

kwenye maangamizi yao.”

26 BwanaMwenye Nguvu Zote atawachapa kwa mjeledi,

kama alivyowapiga Wamidiani

katika mwamba wa Orebu,

naye atainua fimbo yake juu ya maji,

kama alivyofanya huko Misri.

27 Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa

kutoka mabegani mwenu,

na nira yao kutoka shingoni mwenu;

nira itavunjwa

kwa sababu ya kutiwa mafuta.

28 Wanaingia Ayathi,

wanapita katikati ya Migroni,

wanahifadhi mahitaji huko Mikmashi.

29 Wanavuka kivukoni, nao wanasema,

“Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.”

Rama inatetemeka;

Gibea ya Sauli inakimbia.

30 Piga kelele, Ee Binti wa Galimu!

Sikiliza, Ee Laisha!

Maskini Anathothi!

31 Madmena inakimbia;

watu wa Gebimu wanajificha.

32 Siku hii ya leo watasimama Nobu;

watatikisa ngumi zao

katika Mlima wa Binti Sayuni,

katika kilima cha Yerusalemu.

33 Tazama, Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

atayakata matawi kwa nguvu kuu.

Miti mirefu sana itaangushwa,

ile mirefu itashushwa chini.

34 Atakata vichaka vya msitu kwa shoka;

Lebanoni itaanguka mbele zake yeye Mwenye Nguvu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/10-534bef37fc072b5a69f674d40031757a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 × 1 =