Isaya 11

Tawi Kutoka Kwa Yese

1 Chipukizi litatokea kutoka katika shina la Yese,

kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.

2 Roho waBwanaatakaa juu yake,

Roho wa hekima na wa ufahamu,

Roho wa shauri na uweza,

Roho wa maarifa na wa kumchaBwana

3 naye atafurahia kumchaBwana.

Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,

wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,

4 bali kwa adili atahukumu wahitaji,

kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.

Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,

kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.

5 Haki itakuwa mkanda wake

na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.

6 Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,

chui atalala pamoja na mbuzi,

ndama, mwana simba na ng’ombe aliyenona wa mwaka mmoja watalisha pamoja,

naye mtoto mdogo atawaongoza.

7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja,

watoto wao watalala pamoja

na simba atakula majani makavu kama maksai.

8 Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo

la nyoka mwenye sumu kali,

naye mtoto mdogo ataweka mkono wake

kwenye kiota cha nyoka mwenye sumu.

9 Hawatadhuru wala kuharibu

juu ya mlima wangu mtakatifu wote,

kwa kuwa dunia itajawa na kumjuaBwana

kama maji yajazavyo bahari.

10 Katika siku hiyo, shina la Yese litasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa, mataifa yatamkusanyikia na mahali pake pa kupumzika patatukuka.

11 Katika siku hiyo Bwana atanyosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi na kutoka visiwa vya baharini.

12 Atainua bendera kwa mataifa

na kuwakusanya Waisraeli walioko uhamishoni;

atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika

katika pembe nne za dunia.

13 Wivu wa Efraimu utatoweka

na adui wa Yuda watakatiliwa mbali;

Efraimu hatamwonea Yuda wivu

wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.

14 Watawashukia katika mitelemko ya Wafilisti

hadi upande wa magharibi,

kwa pamoja watawateka watu nyara

hadi upande wa mashariki.

Watawapiga Edomu na Moabu,

na Waamoni watatawaliwa nao.

15 Bwanaatakausha

ghuba ya Bahari ya Misri;

kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake

juu ya Mto Eufrati.

Ataugawanya katika vijito saba

ili watu waweze kuuvuka

wakiwa wamevaa viatu.

16 Itakuwepo njia kuu kwa mabaki ya watu wake

wale waliosalia kutoka Ashuru,

kama ilivyokuwa kwa Israeli

walipopanda kutoka Misri.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/11-2d0bea8c3d526964595a3f81ddac2594.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

one + 11 =