Isaya 28

Ole Wa Efraimu

1 Ole wa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu,

kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,

uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba,

kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo!

2 Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu.

Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo uharibuo,

kama mvua inyeshayo kwa nguvu na mafuriko yashukayo,

atakiangusha chini kwa nguvu.

3 Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu,

kitakanyagwa chini ya nyayo.

4 Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake,

uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba,

litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno:

mara mtu aionapo, huichuma na kuila.

5 Katika siku ile,BwanaMwenye Nguvu Zote

atakuwa taji la utukufu,

taji zuri la maua

kwa mabaki ya watu wake.

6 Atakuwa roho ya haki

kwa yeye aketiye katika kiti cha hukumu,

chanzo cha nguvu

kwa wale wazuiao vita langoni.

7 Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo,

wanayumbayumba kwa sababu ya kileo:

Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo,

wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo;

wanapepesuka wanapoona maono,

wanajikwaa wanapotoa maamuzi.

8 Meza zote zimejawa na matapishi

wala hakuna sehemu hata ndogo

isiyokuwa na uchafu.

9 “Yeye anajaribu kumfundisha nani?

Yeye anamwelezea nani ujumbe wake?

Je, ni kwa watoto walioachishwa kunyonya?

Je, ni wale ambao ndipo tu wametolewa matitini?

10 Kwa maana ni:

Amri juu ya amri, amri juu ya amri,

kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni;

hapa kidogo, kule kidogo.”

11 Basi, vyema kabisa, kwa midomo migeni

na kwa lugha ngeni,

Mungu atasema na watu hawa,

12 wale ambao aliwaambia,

“Hapa ni mahali pa kupumzika,

waliochoka na wapumzike,”

na, “Hapa ni mahali pa mapumziko,”

lakini hawakutaka kusikiliza.

13 Hivyo basi, neno laBwanakwao litakuwa:

Amri juu ya amri, amri juu ya amri,

kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni,

hapa kidogo, kule kidogo:

ili waende na kuanguka chali,

wakijeruhiwa, wakinaswa na kukamatwa.

14 Kwa hiyo sikieni neno laBwana,

enyi watu wenye dharau

mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu.

15 Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti,

tumefanya mapatano na kuzimu.

Wakati pigo lifurikalo litakapopita,

haliwezi kutugusa sisi,

kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu

na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.”

16 Kwa hiyo hivi ndivyoBwanaMwenyezi asemavyo:

“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni,

jiwe lililojaribiwa,

jiwe la pembeni la thamani kwa ajili ya msingi thabiti,

yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu.

17 Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia

na uadilifu kuwa timazi;

mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo,

nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha.

18 Agano lenu na kifo litabatilishwa,

patano lenu na kuzimu halitasimama.

Wakati pigo lifurikalo litakapowakumba,

litawaangusha chini.

19 Kila mara lijapo litawachukua,

asubuhi baada ya asubuhi,

wakati wa mchana na wakati wa usiku,

litawakumba tangu mwanzo hadi mwisho.”

Kuuelewa ujumbe huu

utaleta hofu tupu.

20 Kitanda ni kifupi mno kujinyosha juu yake,

nguo ya kujifunikia ni nyembamba mno

mtu asiweze kujifunikia.

21 Bwanaatainuka kama alivyofanya kwenye Mlima Perasimu,

ataghadhibika kama alivyofanya katika Bonde la Gibeoni:

ili kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu,

ili kutimiza kazi yake, kazi yake ngeni.

22 Sasa acheni dharau zenu,

la sivyo minyororo yenu itakuwa mizito zaidi,

Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, ameniambia

habari za maangamizi yaliyoamuriwa dhidi ya nchi yote.

23 Sikilizeni na msikie sauti yangu,

tegeni masikio na msikie niyasemayo.

24 Wakati mkulima alimapo ili apande,

je, hulima siku zote?

Je, huendelea kubomoa ardhi

na kusawazisha udongo?

25 Akiisha kusawazisha shamba,

je, hasii mbegu za bizari na kutawanya jira?

Je, hapandi ngano katika sehemu yake,

shayiri katika eneo lake

na nafaka nyingine katika shamba lake?

26 Mungu wake humwelekeza

na kumfundisha njia iliyo sahihi.

27 Iliki haitwangwi kwa nyundo kubwa,

wala gurudumu la gari halivingirishwi juu ya jira;

iliki hutwangwa kwa mtwangio,

na jira kwa fimbo.

28 Nafaka lazima isagwe ili kutengeneza mkate,

kwa hiyo mtu haendelei kuipura daima.

Ingawa huendesha magurudumu ya gari lake la kupuria juu yake,

farasi wake hawasagi.

29 Haya yote pia hutoka kwaBwanaMwenye Nguvu Zote,

mshauri wa ajabu na anayepita wote kwa hekima.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/28-5e666061cae65be3720839d2b88c5b6d.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

one × four =