Kutoka 25

Sadaka Kwa Ajili Ya Maskani Ya Mungu

1 Bwanaakamwambia Mose,

2 “Waambie Waisraeli waniletee sadaka. Utapokea sadaka kwa ajili yangu kutoka kwa kila mtu ambaye moyo wake wapenda kutoa.

3 Hizi ndizo sadaka utakazozipokea kutoka kwao: dhahabu, fedha na shaba;

4 nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, pamoja na nguo za kitani safi; singa za mbuzi;

5 ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za mbuzi; mbao za mshita;

6 mafuta ya mzeituni kwa ajili ya taa; vikolezi kwa ajili ya mafuta ya kupaka, na kwa ajili ya uvumba wenye harufu nzuri;

7 na vito vya shohamu na vito vingine vya kutiwa kwenye kile kisibau na kifuko cha kifuani.

8 “Kisha amuru watengeneze mahali patakatifu kwa ajili yangu, nami nitakaa miongoni mwao.

9 Tengeneza hema hili na vyombo vyake vyote sawasawa na kielelezo nitakachokuonyesha.

Sanduku La Agano

10 “Nao watatengeneza Sanduku la mbao za mshita, lenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, upana dhiraa moja na nusu, na kimo cha dhiraa moja na nusu.

11 Utalifunika hilo Sanduku kwa dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu juu yake kulizunguka.

12 Utalitengenezea pete nne za dhahabu na kuzifunga kwenye miguu yake minne, pete mbili upande mmoja na pete mbili upande mwingine.

13 Kisha utatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuzifunika kwa dhahabu.

14 Utaiingiza hiyo mipiko kwenye hizo pete zilizo katika pande mbili za hilo Sanduku ili kulibeba.

15 Hiyo mipiko itabakia daima katika hizo pete za hilo Sanduku; haitaondolewa.

16 Kisha weka ndani ya hilo Sanduku ule Ushuhuda nitakaokupa.

17 “Tengeneza kiti cha rehema cha dhahabu safi, chenye urefu wa dhiraa mbili na nusu, na upana wa dhiraa moja na nusu.

18 Tengeneza makerubi wawili kwa dhahabu iliyofuliwa kwenye miisho miwili ya hicho kifuniko.

19 Tengeneza kerubi mmoja kwenye mwisho mmoja, na kerubi mwingine kwenye mwisho mwingine; yatengeneze makerubi yawe kitu kimoja na hicho kifuniko katika miisho hiyo miwili.

20 Makerubi hao watakuwa wametandaza mabawa kuelekea juu, yakitia kivuli hicho kifuniko. Makerubi hao wataelekeana, wakitazama hicho kifuniko.

21 Weka huo Ushuhuda nitakaokupa ndani ya hilo Sanduku la Agano, na uweke hicho kifuniko juu ya hilo Sanduku.

22 Hapo juu ya hicho kifuniko, kati ya hao makerubi wawili walioko juu ya hilo Sanduku la Ushuhuda, hapo ndipo nitakapokutana nawe na kukupa maagizo yangu kwa ajili ya Waisraeli.

Meza Ya Mikate Ya Wonyesho

23 “Tengeneza meza ya mti wa mshita yenye urefu wa dhiraa mbili, upana wa dhiraa moja na kimo cha dhiraa moja na nusu.

24 Ifunike hiyo meza kwa dhahabu safi kisha uifanyie ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote.

25 Kisha tengeneza upapi wenye upana wa nyanda nnena ufanyie ule upapi ukingo kuuzunguka pande zote.

26 Tengeneza pete nne za dhahabu kwa ajili ya meza hiyo, uzifungie kwenye pembe nne, kwenye miguu yake minne.

27 Pete hizo zitakuwa karibu na ukingo ule kushika ile mipiko ambayo ni ya kubebea hiyo meza.

28 Tengeneza mipiko ya mti wa mshita, uifunike dhahabu, hiyo mipiko itakuwa ya kuibebea hiyo meza.

29 Tengeneza sahani zake na masinia yake kwa dhahabu safi, pamoja na bilauri na bakuli zake kwa ajili ya kumiminia sadaka.

30 Utaweka mikate Mitakatifu juu ya meza hii iwe mbele yangu daima.

Kinara Cha Taa

31 “Tengeneza kinara cha taa cha dhahabu safi nacho kiwe cha kazi ya kufua, tako lake na ufito wake; vikombe vyake vinavyofanana na ua, matovu yake na maua yake, vitakuwa vya kitu kimoja.

32 Matawi sita yatatokeza kuanzia ule ufito wa katikati wa kinara cha taa: matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine.

33 Vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi yenye matovu na maua yawe katika tawi moja, matovu matatu katika tawi jingine, na vivyo hivyo kwa matawi yote sita yaliyoanzia kwenye kinara cha taa.

34 Juu ya kinara chenyewe vitakuwepo vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na matovu yake na maua yake.

35 Tovu moja litakuwa chini ya jozi ya kwanza ya matawi yaliyoanzia kwenye kinara cha taa, tovu la pili chini ya jozi ya pili, nalo tovu la tatu chini ya jozi ya tatu, yaani matawi sita kwa jumla.

36 Matovu na matawi yote yatakuwa ya kitu kimoja na kile kinara cha taa vyote vitafuliwa kutoka dhahabu safi.

37 “Kisha tengeneza taa zake saba uziweke juu ya kinara hicho ili ziweze kuangaza mbele yake.

38 Vitu vya kusawazishia vya tambi na vyano, vitakuwa dhahabu safi.

39 Utatumia talanta mojaya dhahabu safi kutengeneza hicho kinara na hivi vifaa vyake vyote.

40 Hakikisha kuwa umevitengeneza sawasawa na kile kielelezo ulichoonyeshwa kule mlimani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/25-a7b6b835771db0a2f88ed1cd7fba41c3.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

19 − 2 =