Kutoka 26

Maskani Ya Mungu

1 “Tengeneza Hema kwa mapazia kumi ya kitani iliyosokotwa vizuri na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, naye fundi stadi atatarizi makerubi kwenye mapazia hayo.

2 Mapazia yote yatakuwa na ukubwa mmoja: kila moja litakuwa na urefu wa dhiraa ishirini na nanena upana wa dhiraa nne.

3 Unganisha mapazia matano kuwa kipande kimoja; fanya vivyo hivyo kwa hayo mengine matano.

4 Tengeneza vitanzi vya kitambaa cha buluu kwenye ukingo wa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, pia kipande cha mwisho cha pazia la pili ufanye vivyo hivyo.

5 Fanya vitanzi hamsini katika pazia la mwisho la kipande cha kwanza na vitanzi hamsini vingine kwenye pazia la mwisho la kipande cha pili, vitanzi vyote vielekeane.

6 Kisha tengeneza kulabu hamsini za dhahabu ili kukaza mapazia pamoja kufanya Hema liwe moja.

7 “Tengeneza mapazia kumi na moja ya singa za mbuzi kwa ajili ya kufunika Hema.

8 Mapazia hayo kumi na moja yatakuwa na kipimo cha aina moja. Kila pazia litakuwa na urefu wa dhiraa thelathini na tatuna upana wa dhiraa nne.

9 Unganisha hayo mapazia matano pamoja na hayo mengine sita pamoja. Kunja hilo pazia la sita mara mbili mbele ya Hema.

10 Tengeneza vitanzi hamsini ukingoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini ukingoni mwa pazia la mwisho la kipande cha pili.

11 Kisha tengeneza kulabu hamsini za shaba, uziingize katika vile vitanzi hamsini ili kukaza Hema kuwa kitu kimoja.

12 Kuhusu kile kipande cha ziada cha pazia la Hema, nusu ya hilo pazia lililobaki litaning’inizwa upande wa nyuma wa Hema.

13 Mapazia ya hema yatakuwa na urefu wa dhiraa moja zaidi pande zote, sehemu itakayobaki itaning’inia pande zote za Hema ili kuifunika.

14 Tengeneza kifuniko cha Hema kwa ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, juu ya kifuniko hicho ufunike ngozi laini za wanyama.

15 “Tengeneza mihimili ya mti wa mshita kwa ajili ya Hema.

16 Kila mhimili uwe na urefu wa dhiraa kumina upana wake dhiraa moja na nusu,

17 ikiwa na ndimi mbili zilizo sambamba. Tengeneza mihimili yote ya Hema jinsi hii.

18 Tengeneza mihimili ishirini ya upande wa kusini wa Hema,

19 kisha tengeneza vitako arobaini vya fedha vya kuweka chini ya hiyo mihimili, vitako viwili kwa kila mhimili, moja chini ya kila ulimi.

20 Kuhusu upande mwingine, yaani upande wa kaskazini wa Hema, tengeneza mihimili ishirini

21 na vitako arobaini vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.

22 Kisha tengeneza mihimili sita kwa kila mwisho, yaani, upande wa magharibi wa Hema,

23 pia utengeneze mihimili miwili ya pembe za mwishoni.

24 Katika pembe hizi mbili ni lazima mihimili iwe miwili kuanzia chini mpaka juu na kushikizwa kwenye pete moja, yote miwili itafanana.

25 Kwa hiyo itakuwepo mihimili minane na vitako kumi na sita vya fedha, viwili chini ya kila mhimili.

26 “Pia tengeneza fito za mti wa mshita: tano kwa ajili ya mihimili ya upande mmoja wa Hema,

27 tano kwa ajili ya mihimili ya upande mwingine, na tano kwa ajili ya mihimili ya upande wa magharibi, mwishoni kabisa mwa Hema.

28 Ufito wa katikati utapenya toka mwisho huu hadi mwisho mwingine katikati ya mihimili.

29 Funika hiyo mihimili kwa dhahabu, kisha tengeneza pete za dhahabu ambazo zitashikilia hizo fito. Pia funika fito hizo kwa dhahabu.

30 “Simamisha Hema sawasawa na ramani uliyoonyeshwa kule juu mlimani.

31 “Tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, naye fundi stadi atarizi makerubi kwenye hayo mapazia.

32 Litundike kwa kulabu za dhahabu kwenye nguzo nne za mti wa mshita ambazo zimefunikwa kwa dhahabu, zikiwa zimesimamishwa kwenye vitako vinne vya fedha.

33 Ning’iniza pazia hilo kwenye vifungo, kisha weka Sanduku la Ushuhuda nyuma ya pazia. Pazia litatenganisha Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu.

34 Weka kifuniko cha kiti cha rehema juu ya Sanduku la Ushuhuda ndani ya mahali Patakatifu pa Patakatifu.

35 Weka meza nje ya pazia upande wa kaskazini wa Hema, kisha weka kinara cha taa upande wa kusini wa Hema.

36 “Kwa ajili ya lango la hema, tengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa vizuri, ambayo ni kazi ya mtarizi.

37 Tengeneza kulabu za dhahabu kwa ajili ya hilo pazia na nguzo tano za mshita zilizofunikwa kwa dhahabu. Kisha mimina vitako vitano vya shaba kwa ajili yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/26-1d653225be8f1117d25d057a148ca0a9.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

13 + nineteen =