Kutoka 28

Mavazi Ya Kikuhani

1 “Mtwae Aroni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.

2 Mshonee Aroni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima.

3 Waambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Aroni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani.

4 Haya ndiyo mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kisibau, kanzu, joho lililorembwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Aroni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.

5 Waambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi.

Kisibau

6 “Tengeneza kisibau cha nyuzi za rangi ya dhahabu, za buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi.

7 Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kisibau.

8 Mshipi wa kiunoni uliotengenezwa kwa ustadi ambao ni kitu kimoja na kisibau utatengenezwa kwa nyuzi za rangi ya dhahabu, za buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, kitani safi iliyosokotwa vizuri.

9 “Chukua mawe mawili ya shohamu na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli

10 kufuatana na walivyozaliwa, majina sita katika jiwe moja na mengine sita katika jiwe jingine.

11 Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya hayo mawe mawili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uyatie hayo mawe katika vijalizo vya dhahabu

12 na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kisibau yawe kama mawe ya kumbukumbu ya wana wa Israeli. Aroni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele zaBwana.

13 Tengeneza vijalizo vya dhahabu

14 na mikufu miwili ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.

Kifuko Cha Kifuani

15 “Fanyiza kifuko cha kifuani kwa ajili ya kufanya maamuzi, kazi ya fundi stadi. Kitengeneze kama kile kisibau: cha nyuzi za rangi ya dhahabu, buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa.

16 Kitakuwa cha mraba, nusu dhiraakila upande, na kikunjwe mara mbili.

17 Kisha weka safu nne za vito vya thamani juu yake. Safu ya kwanza itakuwa ya akiki, yakuti manjano na zabarajadi;

18 katika safu ya pili kitakuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi;

19 safu ya tatu itakuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto;

20 na safu ya nne itakuwa ya krisolitho, shohamu na yaspi. Yote yatiwe kwenye vijalizo vya dhahabu.

21 Patakuwa na mawe kumi na mawili, moja kwa kila jina la wana wa Israeli, kila moja lichorwe kama muhuri likiwa na jina la moja ya makabila kumi na mawili ya Israeli.

22 “Kwa ajili ya kifuko cha kifuani, tengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba.

23 Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili yake uzifungie kwenye pembe mbili za kifuko cha kifuani.

24 Funga ile mikufu miwili ya dhahabu kwenye zile pete zilizo katika pembe za kifuko cha kifuani,

25 zile ncha nyingine mbili za mkufu wa dhahabu zishikamanishe kwenye vijalizo viwili vya kisibau upande wa mbele.

26 Tengeneza pete mbili za dhahabu uzifunge kwenye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kisibau.

27 Tengeneza pete mbili zaidi za dhahabu na uzishikize mbele katika ncha za chini za vipande vya kisibau, mahali kinapoungana juu ya mshipi wa kiunoni wa kisibau.

28 Pete za kifuko cha kifuani zitafungwa pamoja na zile za kisibau kwa kamba ya buluu, ili kiunganishwe na ule mshipi wa kiunoni ili kifuko cha kifuani kisitoke na kuachana na kisibau.

29 “Wakati wo wote Aroni aingiapo Mahali Patakatifu, atakuwa na yale majina ya wana wa Israeli moyoni mwake juu ya kile kifuko cha kifuani cha uamuzi kama kumbukumbu ya kudumu mbele zaBwana.

30 Pia weka Urimu na Thumimundani ya kifuko cha kifuani, yawe juu ya moyo wa Aroni kila mara aingiapo mbele zaBwana. Kwa hiyo siku zote Aroni atakuwa na uwezo kufanya maamuzi kwa ajili ya wana wa Israeli mbele zaBwana.

Mavazi Mengine Ya Kikuhani

31 “Shona kanzu ya kuvalia kisibau kwa kitambaa cha buluu tupu,

32 katikati weka nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe unaofanana na ukosi uliozungushwa kwenye nafasi hiyo ya shingo, ili isichanike.

33 Tengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, weka pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga.

34 Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka pindo la kanzu.

35 Ni lazima Aroni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka katika mahali patakatifu mbele zaBwana, ili asije akafa.

36 “Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore kama muhuri juu yake maneno haya: MTAKATIFU KWABwana.

37 Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba.

38 Aroni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yo yote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Aroni daima ili zikubalike kwaBwana.

39 “Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi.

40 Watengenezee wana wa Aroni makoti, mishipi na kofia, ili kuwapa ukuu na heshima.

41 Baada ya kumvika Aroni ndugu yako pamoja na wanawe nguo hizi, watie mafuta na kuwabariki. Waweke wakfu ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.

42 “Watengenezee nguo za ndani za kitani zitakazofunika mwili, kutoka kiunoni hadi mapajani.

43 Aroni na wanawe ni lazima wavae haya kila wanapoingia katika Hema la Kukutania au wanaposogelea madhabahu wakati wa kutoa huduma mahali patakatifu, ili wasije wakafanya kosa wakafa.

“Haya yawe maagizo ya kudumu kwa Aroni na vizazi vyake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/EXO/28-5675bc9f94b2fe42a79412f3816bc21a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × four =