Luka 11

Yesu Afundisha Wanafunzi Wake Kuomba

1 Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akiomba. Alipomaliza kuomba, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tufundishe kuomba, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.”

2 Akawaambia, “Mnapoomba, semeni hivi:

“ ‘Baba yetu uliye mbinguni,

jina lako litukuzwe,

Ufalme wako uje.

3 Utupatie kila siku riziki zetu.

4 Utusamehe dhambi zetu,

kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea.

Wala usitutie majaribuni,

bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu.’ ”

5 Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu.

6 Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’

7 “Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe cho chote.’

8 Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.

9 “Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni, nanyi mtafunguliwa mlango.

10 Kwa kuwa kila aombaye hupewa, naye kila atafutaye hupata na kila abishaye hufunguliwa mlango.

11 “Je, kuna ye yote miongoni mwenu, ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala ya samaki?

12 Au mtoto akimwomba yai atampa nge?

13 Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”

Yesu Na Beelzebuli

14 Basi Yesu alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu ukashangaa.

15 Lakini wengine wakasema, “Anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebubu, yule mkuu wa pepo wachafu wote.”

16 Wengine ili kumjaribu wakataka awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

17 Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia, nayo nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe huanguka.

18 Kama Shetani amegawanyika mwenyewe ufalme wake utasimamaje? Nawaambia haya kwa sababu ninyi mnadai ya kuwa mimi ninatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli.

19 Kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, wafuasi wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao watakuwa mahakimu wenu.

20 Lakini ikiwa ninatoa pepo wachafu kwa kidole cha Mungu, basi Ufalme wa Mungu umewajia.

21 “Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha, anapoilinda nyumba yake, mali yake iko salama.

22 Lakini mtu mwenye nguvu zaidi kuliko yeye amshambuliapo na kumshinda, humnyang’anya silaha zake zote alizozitegemea na kuchukua nyara.

23 “Mtu ye yote ambaye hayuko pamoja nami, yu kinyume changu na mtu ye yote asiyekusanya pamoja nami, hutapanya.

Kurudi Kwa Pepo Mchafu

24 “Pepo mchafu amtokapo mtu, huzungukazunguka sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini asipopata mahali po pote husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’

25 Arudipo na kuikuta ile nyumba imefagiliwa na kupambwa vizuri,

26 ndipo huenda na kuchukua pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza.”

27 Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”

28 Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

Ishara Ya Yona

29 Umati wa watu ulipokuwa unazidi kuongezeka, Yesu akaendelea kufundisha akisema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara lakini hakitapewa ishara yo yote isipokuwa ile ya Yona.

30 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi cha sasa.

31 Siku ya hukumu, Malkia wa Kusini atainuka pamoja na watu wa kizazi hiki akiwahukumu kwa sababu yeye alisafiri kutoka mbali kuja kusikiliza hekima ya Solomoni. Lakini sasa, yeye aliye mkuu kuliko Solomoni yuko hapa.

32 Siku ile ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu kwa sababu wao walitubu walipomsikia Yona akihubiri. Lakini sasa, yeye aliye mkuu kuliko Yona yuko hapa.

Taa Ya Mwili

33 “Hakuna mtu ye yote awashaye taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunikia chini ya bakuli. Badala yake huiweka juu ya kinara chake, ili watu wote wanaoingia waone nuru.

34 Jicho lako ni taa ya mwili wako. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote umejaa nuru. Lakini kama jicho ni bovu, mwili wako wote umejaa giza.

35 Kwa hiyo, hakikisha kwamba nuru iliyoko ndani yako isiwe giza.

36 Basi ikiwa mwili wako wote umejaa nuru, bila sehemu yake yo yote kuwa gizani, basi utakuwa na nuru kama vile taa ikuangazavyo kwa nuru yake.”

Yesu Awashutumu Mafarisayo Na Wanasheria

37 Yesu alipomaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimkaribisha nyumbani kwake kwa chakula. Yesu akaingia na kuketi katika sehemu yake mezani.

38 Yule Farisayo akashangaa kwamba Yesu hakunawa kwanza kabla ya kula.

39 Ndipo Bwana akamwambia, “Enyi Mafarisayo, mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa choyo na uovu.

40 Enyi wapumbavu! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza nje ndiye aliyetengeneza na ndani pia?

41 Basi toeni sadaka vile mlivyo navyo na tazama, vitu vyote vitakuwa safi kwenu.

42 “Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kutoa matoleo hayo, wala msisahau kufanya hayo mengine.

43 “Ole wenu Mafarisayo, kwa sababu ninyi mnapenda kuketi viti vya mbele katika masinagogi na kusalimiwa kwa heshima masokoni.

44 “Ole wenu, kwa sababu ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.”

45 Mtaalamu mmoja wa sheria akamjibu, akasema, “Mwalimu, unaposema mambo haya, unatutukana na sisi pia.”

46 Yesu akamjibu, “Nanyi wataalamu wa sheria, ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja kuwasaidia.

47 “Ole wenu, kwa sababu ninyi mnawajengea makaburi manabii waliouawa na baba zenu.

48 Hivyo ninyi ni mashahidi na mnathibitisha kile baba zenu walichofanya, wao waliwaua manabii, nanyi mnawatengenezea makaburi.

49 Kwa sababu ya jambo hili, Mungu katika hekima yake alisema, ‘Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na wengine watawatesa.’

50 Kwa hiyo kizazi hiki kitawajibika kwa ajili ya damu ile ya manabii iliyomwagwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu,

51 tangu damu ya Abeli mpaka damu ya Zekaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, nawaambia, kizazi hiki kitawajibika kwa haya yote.

52 “Ole wenu ninyi wataalamu wa sheria, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.”

53 Yesu alipoondoka huko, walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kumpinga vikali na kumsonga kwa maswali,

54 wakivizia kumkamata kwa kitu atakachosema ili wamshtaki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/11-a66d3e7d1fd97cdc08310a982c7537ca.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × 3 =