Luka 10

Yesu Awatuma Wale Sabini Na Wawili

1 Baada ya hayo, Yesu akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda yeye mwenyewe.

2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, awapeleke watenda kazi katika shamba lake.

3 Haya! nendeni. Ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu.

4 Msichukue mkoba wala mfuko, wala viatu na msimsalimu mtu ye yote njiani.

5 “Mkiingia katika nyumba yo yote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’

6 Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake, la sivyo itawarudia.

7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtenda kazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.

8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni cho chote kiwekwacho mbele yenu,

9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’

10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme:

11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakung’uta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’

12 Ninawaambia, hukumu ya Mungu katika Sodoma itavumilika zaidi kuliko ya mji ule.

Ole Wa Miji Isiyotubu

13 “Ole wako Korazini! Ole wake Bethsaida! Kwa kuwa miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika Tiro na Sidoni, ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu.

14 Lakini itavumilika zaidi Tiro na Sidoni katika hukumu kuliko kwenu.

15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.”

16 “Yeye awasikilizaye ninyi, anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi, amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi.

19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui, wala hakuna kitu cho chote kitakachowadhuru kwa namna yo yote.

20 Basi msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Yesu Anashangilia

21 Saa ile ile, Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu akasema, “Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa sababu mambo haya umewaficha wenye hekima na wenye akili, nawe umewafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hayo ndiyo yaliyokuwa mapenzi yako.

22 “Vitu vyote vimekabidhiwa mkononi mwangu na Baba. Wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.”

23 Basi Yesu akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Yamebarikiwa macho yanayoona yale mambo mnayoyaona.

24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona mnayoyaona, lakini hawakuyaona, pia kusikia mnayoyasikia, lakini hawakuyasikia.”

Mfano Wa Msamaria Mwema

25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate kurithi uzima wa milele?”

26 Yesu akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?”

27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote, tena mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”

28 Yesu akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”

29 Lakini yule mtaalamu wa sheria akitaka kuonyesha kuwa mwenye haki, akamwuliza Yesu, “Jirani yangu ni nani?”

30 Yesu akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akitelemka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi, wakampiga, wakaondoka, wakamwacha karibu ya kufa.

31 Kwa bahati nzuri kuhani mmoja alikuwa anapitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.

32 Vivyo hivyo Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani

33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri kupitia njia hiyo alipomwona, alimhurumia,

34 akamwendea, akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake akamleta mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza.

35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbiliakampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yo yote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’

36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu, wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi?”

37 Yule mtaalamu wa sheria akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”

Ndipo Yesu akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”

Yesu Awatembelea Martha Na Maria

38 Ikawa Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani kwake.

39 Martha alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Maria, ambaye yeye aliketi chini miguuni mwa Yesu akisikiliza yale aliyokuwa akisema.

40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Yesu na kumwuliza, “Bwana, hujali kwamba ndugu yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”

41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi?

42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Maria amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/10-f3a38dcbd98e2f9503d5ed7407c6a358.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × 2 =