Luka 18

Mfano Wa Mjane Asiyekata Tamaa

1 Kisha Yesu akawapa wanafunzi wake mfano ili kuwaonyesha kuwa yawapasa kuomba pasipo kukata tamaa.

2 Akawaambia, “Katika mji mmoja alikuwapo hakimu ambaye hakumwogopa Mungu wala kumjali mtu.

3 Katika mji huo alikuwako mjane mmoja ambaye alikuwa akija kwake mara kwa mara akimwomba, ‘Tafadhali nipatie haki kati yangu na adui yangu.’

4 “Kwa muda mrefu yule hakimu alikataa. Lakini hatimaye akasema moyoni mwake, ‘Japokuwa simwogopi Mungu wala simjali mwanadamu,

5 lakini kwa kuwa huyu mjane ananisumbuasumbua, nitahakikisha amepata haki yake ili asiendelee kunichosha kwa kunijia mara kwa mara!’ ”

6 Bwana akasema, “Sikilizeni asemavyo huyu hakimu dhalimu.

7 Je, Mungu hatawatendea haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasaidia?

8 Ninawaambia, atawapatia haki upesi. Lakini je, Mwana wa Adamu atakapokuja ataikuta imani duniani?”

Mfano Wa Farisayo Na Mtoza Ushuru

9 Yesu akatoa mfano huu kwa wale waliojiona kuwa wao ni wenye haki na kuwadharau wengine.

10 “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru.

11 Yule Farisayo, akiwa amesimama peke yake, akasali hivi: ‘Mungu, ninakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine: Wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.

12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma, natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’

13 “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipiga piga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’

14 “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana ye yote ajikwezaye atashushwa na ye yote ajishushaye atakwezwa.”

Yesu Awabariki Watoto Wadogo

15 Pia, watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wachanga ili awaguse. Wanafunzi wake walipoona hivyo, wakawakemea.

16 Lakini Yesu akawaita wale watoto waje kwake, akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu walio kama hawa watoto.

17 Amin, nawaambia, ye yote ambaye hataupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

Mtawala Tajiri

18 Mtawala mmoja akamwuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

19 Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mwema? Hakuna mtu ye yote aliye mwema ila Mungu peke yake.

20 Unazifahamu amri: ‘Usizini, usiue, usiibe, usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

21 Akajibu, “Amri zote hizi nimezishika tangu ujana wangu.”

22 Yesu aliposikia haya, akamwambia, “Bado kuna jambo moja ulilopungukiwa. Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

23 Aliposikia jambo hili, alisikitika sana kwa maana alikuwa mtu mwenye mali nyingi.

24 Yesu akamtazama akasema, “Tazama ni jinsi gani ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!

25 Hakika ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

26 Wale waliosikia haya wakauliza, “Kama ni vigumu hivyo, ni nani basi awezaye kuokoka?”

27 Yesu akajibu, “Yasiyowezekana kwa wanadamu kwa Mungu yawezekana.”

28 Ndipo Petro akasema, “Tazama, tumeacha vyote tulivyokuwanavyo tukakufuata!”

29 Yesu akajibu, “Amin nawaambia, hakuna hata mmoja aliyeacha nyumba yake, au mke, au ndugu, au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu

30 ambaye hatapewa mara nyingi zaidi ya hivyo katika maisha haya na hatimaye kupata uzima wa milele ujao.”

Yesu Kwa Mara Ya Tatu Atabiri Kifo Chake

31 Yesu akawachukua wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia, “Tunapanda kwenda Yerusalemu na kila kitu kilichoandikwa na manabii kumhusu Mwana wa Adamu kitatimizwa.

32 Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa watu wasiomjua Mungu, nao watamdhihaki, watamtukana na kumtemea mate, watampiga mijeledi na kumwua.

33 Siku ya tatu atafufuka.”

34 Wanafunzi wake hawakuelewa mambo haya, kwa kuwa maana yake ilikuwa imefichika kwao, nao hawakujua Yesu alikuwa anazungumzia nini.

Yesu Amponya Kipofu Karibu Na Yeriko

35 Yesu alipokuwa anakaribia Yeriko, kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.

36 Kipofu huyo aliposikia umati wa watu ukipita, akauliza, “Kuna nini?”

37 Wakamwambia, “Yesu wa Nazareti anapita.”

38 Akapaza sauti, akasema, “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu!”

39 Wale waliokuwa wametangulia mbele wakamkemea wakamwambia akae kimya. Lakini yeye akapaza sauti zaidi, “Mwana wa Daudi, unirehemu!”

40 Yesu akasimama, akawaamuru huyo mtu aletwe kwake. Alipokaribia, Yesu akamwuliza,

41 “Unataka nikufanyie nini?”

Akajibu, “Bwana, nataka kuona.”

42 Yesu akamwambia, “Basi upate kuona, imani yako imekuponya.”

43 Akapata kuona saa ile ile, akamfuata Yesu, huku akimsifu Mungu. Watu wote walipoona mambo hayo, nao wakamsifu Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/18-d1f12901b554265eb700b70f240e5a09.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × 2 =