Luka 19

Zakayo Mtoza Ushuru

1 Yesu akaingia Yeriko, naye alikuwa anapita katikati ya huo mji.

2 Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo.

3 Yeye alikuwa akijitahidi kumwona Yesu ni mtu wa namna gani. Lakini kutokana na umati mkubwa wa watu hakuweza kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo.

4 Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati wa watu akapanda juu ya mkuyu ili amwone Yesu, kwa sababu angeipitia njia ile.

5 Yesu alipofika pale chini ya huo mkuyu, akatazama juu, akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani kwako!”

6 Hivyo Zakayo akashuka upesi, akamkaribisha Yesu nyumbani kwake kwa furaha kubwa.

7 Watu wote walioona, wakaanza kunung’unika wakisema, “Amekwenda kuwa mgeni wa ‘mtu mwenye dhambi.’ ”

8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu ye yote kitu cho chote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”

9 Ndipo Yesu akamwambia, “Leo, wokovu umeingia nyumbani humu kwa sababu, huyu naye, ni mwana wa Abrahamu.

10 Kwa maana Mwana wa Adamu amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”

Mfano Wa Fedha

11 Walipokuwa wanasikiliza haya, Yesu akaendelea kuwaambia mfano, kwa sababu alikuwa anakaribia Yerusalemu na watu walikuwa wakidhani ya kuwa Ufalme wa Mungu ulikuwa unakuja saa iyo hiyo.

12 Hivyo akawaambia: “Mtu mmoja mwenye cheo kikubwa, alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi.

13 Hivyo akawaita kumi miongoni mwa watumishi wake akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Fanyeni biashara na fedha hizi mpaka nitakaporudi.’

14 “Lakini raia wa nchi yake walimchukia wakapeleka ujumbe na kusema, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu.’

15 “Hata hivyo alirudi akiwa amekwisha kupokea mamlaka ya ufalme, akawaita wale watumishi wake aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu ni faida kiasi gani kila mmoja wao aliyopata kwa kufanya biashara.

16 “Wa kwanza akaja na kusema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia nimepata faida mara kumi zaidi.’

17 “Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’

18 “Wa pili naye akaja, akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’

19 “Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’

20 “Kisha akaja yule mtumishi mwingine akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa.

21 Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka kitu na unavuna mahali ambapo hukupanda kitu.’

22 “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, nichukuaye mahali ambapo sikuweka kitu na kuvuna mahali ambapo sikupanda,

23 kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba ili nitakaporudi, nichukue iliyo yangu na riba yake?’

24 “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyang’anyeni fungu lake la fedha mkampe yule mwenye kumi.’

25 “Wakamwambia, ‘Bwana, mbona tayari anayo mafungu kumi?’

26 “Akawajibu, ‘Nawaambia kwamba, kila aliye na kitu, ataongezewa, naye yule asiyetumia alicho nacho atanyang’anywa hata kile alicho nacho,

27 lakini wale adui zangu ambao hawakutaka mimi niwe mfalme juu yao, waleteni hapa mkawaue mbele yangu.’ ”

Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Ushindi

28 Baada ya Yesu kusema haya, alitangulia kupanda kwenda Yerusalemu.

29 Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye Mlima uitwao wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili akawaambia,

30 “Nendeni katika kijiji kile kilicho mbele yenu, mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana-punda ambaye hajapandwa na mtu bado, akiwa amefungwa hapo. Mfungueni, mumlete hapa.

31 Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ”

32 Wale waliotumwa wakaenda, wakakuta kila kitu kama vile Yesu alivyokuwa amewaambia.

33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?”

34 Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.”

35 Wakamleta kwa Yesu, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Yesu juu yake.

36 Alipokuwa akienda akiwa amempanda, watu wakatandaza nguo zao barabarani.

37 Alipokaribia mahali yanapoanzia matelemko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema:

38 “Amebarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana!”

“Amani mbinguni na Utukufu huko juu sana.”

39 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwemo miongoni mwa ule umati wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.”

40 Yesu akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapiga kelele.”

Yesu Anaulilia Mji Wa Yerusalemu

41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia,

42 akisema, “Laiti ungalijua hata wewe leo yale ambayo yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako.

43 Hakika siku zinakujia, ambazo adui zako watakuzingira, watakuzunguka pande zote na kukuzuilia ndani.

44 Watakuponda chini, wewe na watoto walioko ndani ya kuta zako. Nao hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kujiliwa kwako.”

Yesu Atakasa Hekaluni

45 Ndipo akaingia Hekaluni akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo.

46 Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala, lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.’ ”

47 Kila siku alikuwa akifundisha Hekaluni. Lakini viongozi wa makuhani, walimu wa sheria na viongozi wa watu walikuwa wakitafuta njia ili kumwua.

48 Lakini hawakupata nafasi kwa sababu watu wote walimfuata wakiyasikiliza maneno yake kwa usikivu mwingi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/19-09a2322e78ac839a7cf7b0ebfc17ee02.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three + 14 =