Luka 3

Yohana Mbatizaji Aanza Kuhubiri

1 Katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato akiwa mtawala wa Uyahudi, Herode akiwa mfalme wa Galilaya, Filipo ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti na Lisania akiwa mfalme wa Abilene,

2 Anasi na Kayafa wakiwa makuhani wakuu, ndipo neno la Mungu likamjia Yohana, mwana wa Zekaria huko nyikani.

3 Akaenda katika nchi yote kandokando ya Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi.

4 Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya:

“Sauti ya mtu aliaye nyikani,

‘Itengenezeni njia ya Bwana,

yanyosheni mapito yake,

5 kila bonde litajazwa,

kila mlima na kilima kitasawazishwa.

Njia zilizopinda zitanyooshwa,

zilizoparuza zitasawazishwa.

6 Nao watu wote watauona

wokovu wa Mungu.’ ”

7 Yohana akauambia ule umati wa watu uliokuwa unakuja ili kubatizwa naye, “Enyi uzao wa nyoka! Ni nani aliyewaonya mwikimbie ghadhabu ijayo?

8 Zaeni matunda yafananayo na toba yenu. Wala msianze kusema mioyoni mwenu kuwa ninyi ni uzao wa Abrahamu. Kwa maana nawaambia, Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka katika mawe haya.

9 Hata sasa shoka limekwisha wekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”

10 Ule umati wa watu ukamwuliza, “Inatupasa tufanyeje basi?”

11 Yohana akawaambia, “Aliye na kanzu mbili amgawie asiye nayo, naye aliye na chakula na afanye vivyo hivyo.”

12 Watoza ushuru nao wakaja ili wabatizwe, wakamwuliza, “Bwana na sisi inatupasa tufanyeje?”

13 Akawaambia, “Msichukue zaidi ya kiwango mlichopangiwa.”

14 Askari nao wakamwuliza, “Je, nasi inatupasa tufanye nini?”

Akawaambia, “Msimdhulumu mtu wala msimshtaki mtu kwa uongo, bali mridhike na mishahara yenu.”

15 Watu walikuwa na matazamio makubwa. Wakawa wanajiuliza mioyoni mwao iwapo Yohana angeweza kuwa ndiye Kristo.

16 Yohana akawajibu akawaambia, “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini atakuja aliye na nguvu kuliko mimi ambaye sistahili hata kufungua kamba ya viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

17 Pepeto lake liko mkononi, tayari kusafisha sakafu yake ya kupuria na kuikusanya ngano ghalani, lakini makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”

18 Basi, kwa maonyo mengine mengi Yohana aliwahubiri watu Habari Njema.

19 Lakini Yohana alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia mke wa ndugu yake na maovu mengine aliyokuwa amefanya,

20 Herode akijumlisha haya yote, akamfunga Yohana gerezani.

Kubatizwa Kwa Bwana Yesu

21 Baada ya watu wote kubatizwa, Yesu naye akabatizwa. Naye alipokuwa akiomba, mbingu zilifunguka.

22 Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa umbo kama la hua na sauti ikaja kutoka mbinguni ikisema: “Wewe ni Mwanangu mpendwa wangu, ninayependezwa nawe sana.”

Ukoo Wa Bwana Yesu

23 Yesu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza huduma yake. Alikuwa akidhaniwa kuwa mwana wa Yosefu,

Yosefu alikuwa mwana wa Eli,

24 Eli alikuwa mwana wa Mathati,

Mathati alikuwa mwana wa Lawi,

Lawi alikuwa mwana wa Melki,

Melki alikuwa mwana wa Yanai,

Yanai alikuwa mwana wa Yosefu,

25 Yosefu alikuwa mwana wa Matathia,

Matathia alikuwa mwana wa Amosi,

Amosi alikuwa mwana wa Nahumu,

Nahumu alikuwa mwana wa Esli,

Esli alikuwa mwana wa Nagai,

26 Nagai alikuwa mwana wa Maathi,

Maathi alikuwa mwana wa Matathia,

Matathia alikuwa mwana Semeini,

Semeini alikuwa mwana wa Yoseki,

Yoseki alikuwa mwana wa Yoda,

27 Yoda alikuwa mwana wa Yoanani,

Yoanani alikuwa mwana wa Resa,

Resa alikuwa mwana wa Zerubabeli,

Zerubabeli alikuwa mwana wa Shealtieli,

Shealtieli alikuwa mwana wa Neri,

28 Neri alikuwa mwana wa Melki,

Melki alikuwa mwana wa Adi,

Adi alikuwa mwana wa Kosamu,

Kosamu alikuwa mwana wa Elmadamu,

Elmadamu alikuwa mwana wa Eri,

29 Eri alikuwa mwana wa Yoshua,

Yoshua alikuwa mwana wa Eliezeri,

Eliezeri alikuwa mwana wa Yorimu,

Yorimu alikuwa mwana wa Mathati,

Mathati alikuwa mwana wa Lawi,

30 Lawi alikuwa mwana wa Simeoni,

Simeoni alikuwa mwana wa Yuda,

Yuda alikuwa mwana wa Yosefu,

Yosefu alikuwa mwana wa Yonamu,

Yonamu alikuwa mwana wa Eliakimu,

Eliyakimu alikuwa mwana wa Melea,

31 Melea alikuwa mwana wa Mena,

Mena alikuwa mwana wa Matatha,

Matatha alikuwa mwana wa Nathani,

Nathani alikuwa mwana wa Daudi,

32 Daudi alikuwa mwana wa Yese,

Yese alikuwa mwana wa Obedi,

Obedi alikuwa mwana wa Boazi,

Boazi alikuwa mwana wa Salmoni,

Salmoni alikuwa mwana wa Nashoni,

33 Nashoni alikuwa mwana wa Aminadabu,

Aminadabu alikuwa mwana wa Aramu,

Aramu alikuwa mwana wa Hesroni,

Hesroni alikuwa mwana wa Peresi,

Peresi alikuwa mwana wa Yuda,

34 Yuda alikuwa mwana wa Yakobo,

Yakobo alikuwa mwana wa Isaki,

Isaki alikuwa mwana wa Abrahamu,

Abrahamu alikuwa mwana wa Tera,

Tera alikuwa mwana wa Nahori,

35 Nahori alikuwa mwana wa Serugi,

Serugi alikuwa mwana wa Reu,

Reu alikuwa mwana wa Pelegi,

Pelegi alikuwa mwana wa Eberi,

Eberi alikuwa mwana wa Sala,

36 Sala alikuwa mwana wa Kenani,

Kenani alikuwa mwana wa Arfaksadi,

Arfaksadi alikuwa mwana wa Shemu,

Shemu alikuwa mwana wa Noa,

Noa alikuwa mwana wa Lameki,

37 Lameki alikuwa mwana wa Methusela,

Methusela alikuwa mwana wa Enoki,

Enoki alikuwa mwana wa Yaredi,

Yaredi alikuwa mwana wa Mahalaleli,

Mahalaleli alikuwa mwana wa Kenani,

38 Kenani alikuwa mwana wa Enoshi,

Enoshi alikuwa mwana wa Sethi,

Sethi alikuwa mwana wa Adamu,

Adamu alikuwa mwana wa Mungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/3-4f24e97fdb3888418e406480ddd41e65.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

19 − fourteen =