Luka 4

Yesu Ajaribiwa Na Shetani

1 Yesu, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akarudi kutoka Yordani akaongozwa na Roho Mtakatifu hadi jangwani,

2 mahali ambako kwa siku arobaini alikuwa akijaribiwa na ibilisi. Kwa siku zote hizo hakula cho chote, hivyo baada ya muda huo akaona njaa.

3 Ibilisi akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”

4 Yesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno la Mungu.’ ”

5 Ibilisi akampeleka hadi juu ya mlima mrefu akamwonyesha milki zote za dunia kwa mara moja.

6 Akamwambia, “Nitakupa mamlaka juu ya milki hizi na fahari zake zote, kwa maana zimekabidhiwa mkononi mwangu nami ninaweza kumpa ye yote ninayetaka.

7 Hivyo ikiwa utanisujudia na kuniabudu, vyote vitakuwa vyako.”

8 Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake.’ ”

9 Kisha ibilisi akampeleka mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya mnara mrefu mwembamba wa Hekalu, akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa,

10 kwa maana imeandikwa:

“ ‘Atakuagizia malaika zake

ili wakulinde;

11 nao watakuchukua mikononi mwao

usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”

12 Yesu akamjibu, “Imesemwa, ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

13 Ibilisi alipomaliza kila jaribu, akamwacha Yesu mpaka wakati mwingine ufaao.

Mwanzo Wa Huduma Ya Galilaya

14 Kisha Yesu akarudi mpaka Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando.

15 Akaanza kufundisha kwenye masinagogi yao na kila mmoja akamsifu.

Kukataliwa Kwa Yesu

16 Yesu akaenda Nazareti, hapo alipolelewa na siku ya Sabato alikwenda katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome,

17 naye akapewa kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na kukuta mahali palipoandikwa:

18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,

kwa sababu amenitia mafuta

kuwaletea maskini habari njema.

Amenituma kuwatangazia wafungwa

kufunguliwa kwao

na vipofu kupata kuona tena,

kuwaweka huru wanaoonewa

19 na kutangaza mwaka wa Bwana

uliokubalika.”

20 Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi na akaketi. Watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho.

21 Ndipo akaanza kwa kuwaambia, “Leo maandiko haya yametimia mkiwa mnasikia.”

22 Wote waliokuwako wakamsifu na kuyastaajabia maneno yake yaliyojaa neema, wakaulizana, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”

23 Yesu akawaambia, “Bila shaka mtatumia mithali hii, ‘Tabibu, jiponye mwenyewe! Mambo yale tuliyosikia kwamba uliyafanya huko Kapernaumu, yafanye na hapa kwenye mji wako.’ ”

24 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna nabii anayekubalika kwenye mji wake mwenyewe.

25 Lakini ukweli ni kwamba palikuwa na wajane wengi katika Israeli wakati wa Eliya, mbingu zilipofungwa kwa miaka mitatu na miezi sita pakawa na njaa kuu katika nchi nzima.

26 Hata hivyo Eliya hakutumwa hata kwa mmoja wao, bali kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni.

27 Pia palikuwa na wengi wenye ukoma katika Israeli katika siku za nabii Elisha, lakini hakuna hata mmoja wao aliyetakaswa, isipokuwa Naamani mtu wa Shamu.”

28 Watu wote katika sinagogi waliposikia maneno haya, wakakasirika sana.

29 Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakamchukua hadi kwenye kilele cha mlima mahali ambapo mji huo ulikuwa umejengwa, ili wamtupe chini kutoka kwenye mtelemko mkali.

30 Lakini yeye akapita papo hapo katikati ya huo umati wa watu akaenda zake.

Yesu Atoa Pepo Mchafu

31 Kisha Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya na katika siku ya Sabato akawa anafundisha.

32 Wakashangazwa sana na mafundisho yake, maana maneno yake yalikuwa na mamlaka.

33 Ndani ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, akapiga kelele kwa nguvu akisema,

34 “Tuache! Tuna nini nawe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakujua wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.”

35 Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza na umtoke!” Yule pepo mchafu akamwangusha chini yule mtu mbele yao wote, akatoka pasipo kumdhuru.

36 Watu wote wakashangaa wakaambiana, “Mafundisho haya ni ya namna gani? Kwa mamlaka na nguvu, anawaamuru pepo wachafu, nao wanatoka!”

37 Habari zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu ile.

Yesu Awaponya Wengi

38 Yesu akatoka kwenye sinagogi akaenda nyumbani kwa Simoni. Basi huko alimkuta mkwewe Simoni ana homa kali, nao wakamwomba Yesu amsaidie.

39 Hivyo Yesu akamwinamia na kukemea ile homa, nayo ikamwacha. Akaamka saa ile ile akaanza kuwahudumia.

40 Jua lilipokuwa linatua, watu wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali wakawaleta kwa Yesu, naye akaweka mikono yake juu ya kila mgonjwa, akawaponya.

41 Pepo wachafu pia wakawatoka watu wengi, nao walipokuwa wakitoka wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea na kuwazuia wasiseme, kwa maana walimjua kuwa yeye ni Kristo.

42 Kesho yake, kulipopambazuka, Yesu alikwenda mahali pa faragha. Watu wengi wakawa wanamtafuta kila mahali, nao walipomwona wakajaribu kumzuia asiondoke.

43 Lakini yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”

44 Naye aliendelea kuhubiri katika masinagogi ya Uyahudi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/4-74d9ef592c42d3263c1c569544d928cf.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

5 + thirteen =