Mambo ya Walawi 14

Kutakasa Kutoka Maambukizo Ya Magonjwa Ya Ngozi

1 Bwanaakamwambia Mose,

2 “Haya ndiyo masharti yamhusuyo mtu mgonjwa wakati wa kufanyiwa ibada ya utakaso wakati aletwapo kwa kuhani:

3 Kuhani atakwenda kumchunguza nje ya kambi. Kama mtu huyo atakuwa amepona ugonjwa wake wa ngozi wa kuambukiza,

4 kuhani ataagiza vitu vifuatavyo viletwe kwa ajili ya mtu atakayetakaswa: ndege wawili safi walio hai, mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo.

5 Kisha kuhani ataagiza kwamba mmoja wa ndege wale achinjwe kwenye chungu chenye maji safi.

6 Kisha kuhani atamchukua ndege aliye hai na kumtumbukiza pamoja na mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo ndani ya damu ya yule ndege aliyechinjiwa kwenye maji safi.

7 Atamnyunyizia yule mwenye ugonjwa wa kuambukiza maji hayo mara saba na kumtangaza kuwa safi. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai aende zake kwenye mashamba.

8 “Huyo mtu atakayetakaswa ni lazima afue nguo zake, anyoe nywele zake zote, na aoge kwa maji; ndipo atakapokuwa safi kwa desturi ya ibada. Baada ya hili anaweza kuingia kambini, lakini ni lazima akae nje ya hema lake kwa siku saba.

9 Siku ya saba ni lazima anyoe nywele zake zote; yaani anyoe nywele za kichwa, ndevu zake, kope zake na nywele nyingine zote. Ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa safi.

10 “Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja, na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi za efaza unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi mojaya mafuta.

11 Kuhani atakayemtangaza kuwa safi atahitaji kumkabidhi mgonjwa aliyepona pamoja na sadaka zake zote mbele zaBwanakatika ingilio la Hema la Kukutania.

12 “Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele zaBwanakuwa sadaka ya kuinuliwa.

13 Atamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; nayo ni takatifu sana.

14 Kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wa kuume.

15 Kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, atamimina kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto,

16 atachovya kidole chake cha mkono wa kuume kwenye mafuta yaliyoko kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho atamnyunyizia mtu yule anayetakaswa mara saba mbele zaBwana.

17 Kuhani atampaka sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wa kuume, mahali pale pale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia.

18 Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele zaBwana.

19 “Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa

20 na kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi.

21 “Hata hivyo, kama ni maskini na hawezi kupata vitu hivi, ni lazima achukue mwana-kondoo mmoja kama sadaka ya hatia ipate kuinuliwa ili kumfanyia upatanisho pamoja na sehemu ya kumi ya efaya unga laini uliochanganywa na logi moja ya mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka,

22 na hua wawili au makinda mawili ya njiwa, kile atakachoweza kupata, mmoja kwa sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa.

23 “Katika siku ya nane ni lazima avilete vitu hivyo kwa kuhani, kwa ajili ya kutakaswa kwake kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele zaBwana.

24 Kuhani atamchukua mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia pamoja na ile logi ya mafuta ya kuinuliwa mbele zaBwanakuwa sadaka ya kuinuliwa.

25 Atamchinja huyo mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia pia ataichukua sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, ataipaka pia kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wa kuume.

26 Kuhani atamiminia sehemu ya mafuta kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto,

27 na kwa kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume, atamnyunyizia yule anayetakaswa yale mafuta yaliyo kwenye kiganja chake mara saba mbele zaBwana.

28 Atampaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake katika sehemu zote kama alivyompaka damu ya sadaka ya hatia: yaani, kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wa kuume.

29 Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki katika kiganja chake kwenye kichwa cha yule anayetakaswa na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele zaBwana.

30 Kisha atatoa dhabihu wale hua ama yale makinda ya njiwa, ambayo mtu ataweza kuwapata,

31 mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya nafaka. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho mbele zaBwanakwa ajili ya yule anayetakaswa.”

32 Haya ndiyo masharti kwa mtu ye yote mwenye ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza na ambaye hana uwezo wa kutoa sadaka za kawaida kwa ajili ya kutakaswa kwake.

Kutakaswa Upele

33 Bwanaakamwambia Mose na Aroni,

34 “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ambayo ninawapa kuwa milki yenu, nami nikaweka upele ueneao kwenye nyumba katika nchi ile,

35 ni lazima mwenye nyumba hiyo akamwambie kuhani, ‘Nimeona kitu fulani kinachofanana na upele kwenye nyumba yangu.’

36 Kuhani ataagiza vitu vyote vitolewe ndani ya nyumba kabla hajaenda kuchunguza kama ina ugonjwa huo, ili kitu cho chote ndani ya nyumba kisitangazwe kuwa najisi. Baada ya hili kuhani ataingia ndani na kuikagua hiyo nyumba.

37 Atachunguza upele huo katika kuta za nyumba hiyo, nazo kama zina rangi ya kijani kibichi au wekundu na kuna mibonyeo ndani ya ukuta,

38 kuhani atatoka na kufunga mlango wa nyumba hiyo kwa siku saba.

39 Siku ya saba, kuhani atarudi kuikagua nyumba. Kama upele umeenea juu ya kuta,

40 ataagiza kwamba mawe yote yaliyoambukizwa yaondolewe na kutupwa katika eneo lililo najisi nje ya mji.

41 Kuta zote za ndani ya nyumba hiyo ni lazima zikwanguliwe na kifusi chake kitupwe mahali najisi nje ya mji.

42 Kisha watachukua mawe mengine na kujenga palipobomolewa kwa udongo mpya wa mfinyanzi na kuipiga nyumba hiyo lipu mpya.

43 “Ikiwa upele huo utatokea tena ndani ya ile nyumba baada ya mawe kuondolewa na nyumba kukwanguliwa na kuwekwa lipu mpya,

44 kuhani atakwenda kuikagua na kama upele umeenea ndani ya nyumba, basi ni upele uharibuo; nyumba hiyo ni najisi.

45 Ni lazima ibomolewe: mawe yake, mbao na lipu yake, vikatupwe nje ya mji mahali palipo najisi.

46 “Ye yote atakayeingia katika nyumba hiyo ikiwa imefungwa atakuwa najisi mpaka jioni.

47 Ye yote atakayelala au kula ndani ya nyumba hiyo ni lazima afue nguo zake.

48 “Lakini ikiwa kuhani atakuja kuikagua na kukuta kuwa upele haujaenea tena baada ya nyumba kupigwa lipu, ataitangaza nyumba ile kuwa safi, kwa sababu upele umekwisha.

49 Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili, mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo.

50 Atamchinja mmoja wa wale ndege kwenye chungu chenye maji safi.

51 Kisha atachukua mti wa mwerezi, hisopo, kitani nyekundu na ndege aliye hai na kuvitumbukiza ndani ya damu ya ndege aliyechinjwa pamoja na maji safi na kuinyunyizia nyumba ile mara saba.

52 Ataitakasa nyumba kwa damu ya yule ndege, maji safi, ndege aliye hai, mti wa mwerezi, hisopo na kitani nyekundu.

53 Kisha atamwachia yule ndege aliye hai huru mashambani nje ya mji. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ile, nayo itakuwa safi.”

54 Haya ndiyo masharti kuhusu aina yo yote ya ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, mwasho wo wote,

55 upele ndani ya nguo au ndani ya nyumba,

56 kwa uvimbe, vipele au kipaku king’aacho,

57 kupambanua wakati kitu fulani ni safi au najisi.

Haya ndiyo masharti kuhusu magonjwa ya ngozi ya kuambukiza na upele.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LEV/14-351a09a6716335fa75a860e093bd21a8.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty + eleven =