Maombolezo 1

1 Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa,

mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu!

Jinsi ambavyo umekuwa kama mama mjane,

ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa!

Yule ambaye alikuwa malkia miongoni mwa majimbo

sasa amekuwa mtumwa.

2 Kwa uchungu, hulia sana usiku,

machozi yapo kwenye mashavu yake.

Miongoni mwa wapenzi wake wote

hakuna ye yote wa kumfariji.

Rafiki zake wote wamemsaliti,

wamekuwa adui zake.

3 Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili,

Yuda amekwenda uhamishoni.

Anakaa miongoni mwa mataifa,

hapati mahali pa kupumzika.

Wote ambao wanamsaka wamemkamata

katikati ya dhiki yake.

4 Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza,

kwa kuwa hakuna ye yote anayekuja

kwenye sikukuu zake zilizoamriwa.

Malango yake yote yamekuwa ukiwa,

makuhani wake wanalia kwa uchungu,

wanawali wake wanahuzunika,

naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu.

5 Adui zake wamekuwa mabwana zake,

watesi wake wana raha.

Bwanaamemletea huzuni

kwa sababu ya dhambi zake nyingi.

Watoto wake wamekwenda uhamishoni,

mateka mbele ya adui.

6 Fahari yote imeondoka

kutoka kwa Binti Sayuni.

Wakuu wake wako kama ayala

ambaye hapati malisho,

katika udhaifu wamekimbia

mbele ya anayewasaka.

7 Katika siku za mateso yake na kutangatanga

Yerusalemu hukumbuka hazina zote

ambazo zilikuwa zake katika siku za kale.

Wakati watu wake walipoanguka katika mikono ya adui,

hapakuwepo na ye yote wa kumsaidia.

Watesi wake walimtazama

na kumcheka katika maangamizi yake.

8 Yerusalemu ametenda dhambi sana

kwa hiyo amekuwa najisi.

Wote waliomheshimu wanamdharau,

kwa maana wameuona uchi wake,

yeye mwenyewe anapiga kite

na kugeukia mbali.

9 Uchafu wake umegandamana na nguo zake;

hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye.

Anguko lake lilikuwa la kushangaza,

hapakuwepo na ye yote wa kumfariji.

“Tazama, EeBwana, teso langu,

kwa maana adui ameshinda.”

10 Adui ametia mikono

juu ya hazina zake zote,

aliona mataifa yakipagani

wakiingia mahali patakatifu pake,

wale uliowakataza kuingia

kwenye kusanyiko lako.

11 Watu wake wote wanalia kwa uchungu

watafutapo chakula;

wanabadilisha hazina zao kwa chakula

ili waweze kuendelea kuishi.

“Tazama, EeBwana, ufikiri,

kwa maana nimedharauliwa.”

12 “Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando?

Angalieni kote muone.

Je, kuna maumivu kama maumivu yangu

yale yaliyotiwa juu yangu,

yaleBwanaaliyoyaleta juu yangu

katika siku ya hasira yake kali?

13 “Kutoka juu alipeleka moto,

akaushusha katika mifupa yangu.

Aliitandia wavu miguu yangu

na akanirudisha nyuma.

Akanifanya mkiwa,

na mdhaifu mchana kutwa.

14 “Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira,

kwa mikono yake zilifumwa pamoja.

Zimefika shingoni mwangu

na Bwana ameziondoa nguvu zangu.

Amenitia mikononi mwa wale

ambao siwezi kushindana nao.

15 “Bwana amewakataa wapiganaji wa vita

wote walio kati yangu,

ameagiza jeshi dhidi yangu

kuwaponda vijana wangu wa kiume.

Katika shinikizo lake la divai Bwana amemkanyaga

Bikira Binti Yuda.

16 “Hii ndiyo sababu ninalia

na macho yangu yanafurika machozi.

Hakuna ye yote aliye karibu kunifariji,

hakuna ye yote wa kuhuisha roho yangu.

Watoto wangu ni wakiwa

kwa sababu adui ameshinda.”

17 Sayuni ananyosha mikono yake,

lakini hakuna ye yote wa kumfariji.

Bwanaametoa amri kwa ajili ya Yakobo

kwamba majirani zake wawe adui zake;

Yerusalemu umekuwa

kitu najisi miongoni mwao.

18 “Bwanani mwenye haki,

hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake.

Sikilizeni, enyi mataifa yote,

tazameni maumivu yangu.

Wavulana wangu na wasichana wangu

wamekwenda uhamishoni.

19 “Niliita washirika wangu

lakini walinisaliti.

Makuhani wangu na wazee wangu

waliangamia mjini

walipokuwa wakitafuta chakula

ili waweze kuishi.

20 “Angalia, EeBwana, jinsi nilivyo katika dhiki!

Nina maumivu makali ndani yangu,

nami ninahangaika moyoni mwangu,

kwa kuwa nimekuwa mwasi sana.

Huko nje, upanga unaua watu,

ndani, kipo kifo tu.

21 “Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu,

lakini hakuna ye yote wa kunifariji.

Adui zangu wote wamesikia juu ya dhiki yangu,

wanafurahia lile ulilolitenda.

Naomba uilete siku uliyoitangaza

ili wawe kama mimi.

22 “Uovu wao wote na uje mbele zako;

uwashughulikie wao

kama vile ulivyonishughulikia mimi

kwa sababu ya dhambi zangu zote.

Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi

na moyo wangu umedhoofika.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LAM/1-fe84efa99093d520960c29d74e38ee5e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

seventeen − 13 =