Maombolezo 2

1 Tazama jinsi Bwana alivyomfunika Binti Sayuni

kwa wingu la hasira yake!

Ameitupa chini fahari ya Israeli

kutoka mbinguni mpaka duniani,

hakukumbuka kiti chake cha kuwekea miguu

katika siku ya hasira yake.

2 Bila huruma Bwana ameyameza

makao yote ya Yakobo;

katika ghadhabu yake amebomoa

ngome za Binti Yuda.

Ameuangusha ufalme wake na wakuu wake

chini kwa aibu.

3 Katika hasira kali amevunja

# kila pembeya Israeli.

Ameuondoa mkono wake wa kuume

alipokaribia adui.

Amemteketeza Yakobo kama moto uwakao

ule uteketezao kila kitu kinachouzunguka.

4 Ameupinda upindi wake kama adui,

mkono wake wa kuume uko tayari.

Kama vile adui amewachinja

wote waliokuwa wanapendeza jicho,

amemwaga ghadhabu yake kama moto

juu ya hema la Binti Sayuni.

5 Bwana ni kama adui;

amemmeza Israeli.

Amemeza majumba yake yote ya kifalme

na kuangamiza ngome zake.

Ameongeza huzuni na maombolezo

kwa ajili ya Binti Yuda.

6 Ameharibu maskani yake kama bustani,

ameharibu mahali pake pa mkutano.

Bwanaamemfanya Sayuni kusahau

sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake;

katika hasira yake kali amewakataa kwa dharau

mfalme na kuhani.

7 Bwana amekataa madhabahu yake

na kuacha mahali patakatifu pake.

Amemkabidhi adui kuta

za majumba yake ya kifalme;

wamepiga kelele katika nyumba yaBwana

kama katika siku ya sikukuu iliyoamuriwa.

8 Bwanaalikusudia kuangusha

ukuta uliomzunguka Binti Sayuni.

Ameinyoosha kamba ya kupimia

na hakuuzuia mkono wake usiangamize.

Alifanya maboma na kuta ziomboleze,

vyote vikaharibika pamoja.

9 Malango yake yamezama ardhini,

makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu.

Mfalme wake na wakuu wake

wamepelekwa uhamishoni

miongoni mwa mataifa,

sheria haipo tena,

na manabii wake hawapati tena

maono kutoka kwaBwana.

10 Wazee wa Binti Sayuni

wanaketi chini kimya,

wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao

na kuvaa nguo za gunia.

Wanawali wa Yerusalemu

wamesujudu hadi ardhini.

11 Macho yangu yamedhoofika kwa kulia,

nina maumivu makali ndani,

moyo wangu umemiminwa ardhini

kwa sababu watu wangu wameangamizwa,

kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia

kwenye barabara za mji.

12 Wanawaambia mama zao,

“Wapi mkate na divai?”

Wazimiapo kama watu waliojeruhiwa

katika barabara za mji,

maisha yao yadhoofikavyo

mikononi mwa mama zao.

13 Ninaweza kusema nini kwa ajili yako?

Nikulinganishe na nini,

Ee Binti Yerusalemu?

Nitakufananisha na nini,

ili nipate kukufariji,

Ee Bikira Binti Sayuni?

Jeraha lako lina kina kama bahari.

Ni nani awezaye kukuponya?

14 Maono ya manabii wako

yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu,

hawakuifunua dhambi yako

katika kuzuilia kwenda kwako utumwani.

Maneno waliyokupa

yalikuwa ya uongo na ya kupotosha.

15 Wote wapitiao njia yako

hukupigia makofi,

wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao

kwa Binti Yerusalemu:

“Huu ndio ule mji ulioitwa

mkamilifu wa uzuri,

furaha ya dunia yote?”

16 Adui zako wote wanapanua

vinywa vyao dhidi yako,

wanadhihaki na kusaga meno yao

na kusema, “Tumemmeza.

Hii ndiyo siku tuliyoingojea,

tumeishi na kuiona.”

17 Bwanaamefanya lile alilolipanga;

ametimiza neno lake

aliloliamuru siku za kale.

Amekuangusha bila huruma,

amewaacha adui wakusimange,

ametukuza pembe ya adui yako.

18 Mioyo ya watu

inamlilia Bwana.

Ee ukuta wa Binti Sayuni,

machozi yako na yatiririke kama mto

mchana na usiku;

usijipe nafuu,

macho yako yasipumzike

19 Inuka, lia usiku,

zamu za usiku zianzapo;

mimina moyo wako kama maji

mbele za Bwana.

Mwinulie yeye mikono yako

kwa ajili ya maisha ya watoto wako,

ambao wanazimia kwa njaa

kwenye kila mwanzo wa barabara.

20 “Tazama, EeBwana, ufikirie:

Ni nani ambaye umepata

kumtendea namna hii?

Je, wanawake wale wazao wao,

watoto waliowalea?

Je, kuhani na nabii auawe

mahali patakatifu pa Bwana?

21 “Vijana na wazee hujilaza pamoja

katika mavumbi ya barabarani,

wavulana wangu na wasichana

wameanguka kwa upanga.

Umewaua katika siku ya hasira yako,

umewachinja bila huruma.

22 “Kama ulivyoita siku ya karamu,

ndivyo ulivyoagiza hofu kuu

dhidi yangu kila upande.

Katika siku ya hasira yaBwana

hakuna ye yote aliyekwepa au kupona;

wale niliowatunza na kuwalea,

adui yangu amewaangamiza.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LAM/2-cb20a5aaf59c8cada0cbd201bf7e3125.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

19 + 3 =