Marko 10

Mafundisho Kuhusu Talaka

1 Yesu akaondoka huko akavuka Mto wa Yordani, akaenda sehemu ya Uyahudi. Umati mkubwa wa watu ukamjia tena na kama ilivyokuwa desturi yake akawafundisha.

2 Baadhi ya Mafarisayo wakaja ili kumjaribu kwa kumwuliza, “Je, ni halali mtu kumwacha mke wake?”

3 Yesu akawajibu, “Je, Mose aliwaamuru nini?”

4 Wakajibu, “Mose aliruhusu kwamba mume anaweza kumwandikia mkewe hati ya talaka na kumwacha.”

5 Yesu akawaambia, “Mose aliwaandikia sheria hiyo kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.

6 Lakini tangu mwanzo wa uumbaji, ‘Mungu aliwaumba mume na mke.

7 Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe na hao wawili, watakuwa mwili mmoja.’

8 Kwa hiyo hawatakuwa wawili tena bali mwili mmoja.

9 Basi, alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

10 Walipokuwa tena ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza kuhusu jambo hili.

11 Akawajibu, “Mtu ye yote anayemwacha mkewe na kuoa mke mwingine, azini naye.

12 Naye mwanamke anayemwacha mumewe na kuolewa na mume mwingine, anazini.”

Yesu Anawabariki Watoto Wadogo

13 Watu walikuwa wakimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse lakini wanafunzi wake wakawakemea.

14 Yesu alipoona yaliyokuwa yakitukia akachukizwa, akawaambia wanafunzi wake, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wa watu kama hawa.

15 Amin, amin nawaambia, mtu ye yote asiyeukubali Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hatauingia kamwe.”

16 Akawachukua watoto mikononi mwake, akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

Kijana Tajiri

17 Yesu alipokuwa anaondoka, mtu mmoja akamkimbilia, akapiga magoti mbele yake, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”

18 Yesu akamwambia, “Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema isipokuwa Mungu peke yake.

19 Unazijua amri: ‘Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, usidanganye, waheshimu baba yako na mama yako.’ ”

20 Akamjibu, “Mwalimu, amri hizi zote nimezishika tangu nikiwa mtoto.”

21 Yesu akamtazama na kumpenda, akamwambia, “Umepungukiwa na kitu kimoja, nenda ukauze kila kitu ulicho nacho uwape maskini hizo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

22 Yule mtu aliposikia hayo, akasikitika sana, akaondoka kwa huzuni kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

23 Yesu akatazama pande zote, akawaambia wanafunzi wake, “Itakuwa vigumu sana kwa wenye mali kuingia kwenye Ufalme wa Mungu!”

24 Wanafunzi wake wakashangazwa sana na maneno hayo. Lakini Yesu akawaambia tena, “Wanangu, tazama jinsi ilivyo vigumu kwa wale wanaotumainia mali kuingia katika Ufalme wa Mungu.

25 Ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko tajirikuingia katika Ufalme wa Mungu.”

26 Wanafunzi wake wakashangaa mno. Wakaulizana wao kwa wao, “Ni nani basi awezaye kuokolewa?”

27 Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu hili haliwezekani, lakini kwa Mungu sivyo. Yote kwa Mungu yanawezekana.”

28 Petro akaanza kumwambia, “Tazama, tumeacha kila kitu na kukufuata wewe!”

29 Yesu akasema, “Amin, nawaambia, hakuna mtu ye yote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume, au ndugu wa kike, mama, baba, watoto au mashamba kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili,

30 ambaye hatalipwa mara mia katika ulimwengu huu, nyumba, ndugu wa kiume, ndugu wa kike, mama, baba, watoto, mashamba pamoja na mateso, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”

Yesu Atabiri Mara Ya Tatu Kufa Na Kufufuka Kwake

32 Walikuwa njiani wakipanda kwenda Yerusalemu na Yesu alikuwa ametangulia. Wanafunzi wake walishangaa, nao watu waliowafuata walijawa na hofu. Yesu akawachukua tena wale wanafunzi wake kumi na wawili kando na kuwaambia yatakayompata.

33 Akasema, “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atasalitiwa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Wao watamhukumu kifo na kumtia mikononi mwa watu Mataifa,

34 ambao watamdhihaki, watamtemea mate, watampiga na kumwua. Siku tatu baada ya kifo chake atafufuka.”

Ombi La Yakobo Na Yohana

35 Kisha Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakaja mbele alikokuwa na kumwambia, “Mwalimu, tunataka utufanyie lo lote tutakalokuomba.”

36 Naye akawaambia, “Je, mwataka niwafanyie jambo gani?”

37 Wakamwambia, “Tupe kukaa mmoja upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto katika utukufu wako.”

38 Lakini Yesu akawaambia, “Hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi?”

39 Wakajibu, “Tunaweza.”

Kisha Yesu akawaambia, “Kikombe nikinyweacho mtakinywea na ubatizo nibatizwao mtabatizwa,

40 lakini kuketi mkono wangu wa kuume au wa kushoto si juu yangu mimi kuwapa. Nafasi hizi ni kwa ajili ya wale walioandaliwa.”

41 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana.

42 Yesu akawaita wanafunzi wake pamoja akawaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu Mataifa huwatawala watu kwa nguvu, nao wenye vyeo huwaonyesha mamlaka yao.

43 Lakini sivyo kwenu. Badala yake ye yote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu

44 na ye yote anayetaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa mtumwa wa wote.

45 Kwa kuwa hata Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake kuwa ukombozi kwa ajili ya wengi.”

Yesu Amponya Kipofu Bartimayo

46 Kisha wakafika Yeriko. Wakati Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu mmoja, jina lake Bartimayo, mwana wa Timayo, alikuwa ameketi kando ya njia akiomba msaada.

47 Aliposikia kuwa ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita, akaanza kupaza sauti akisema, “Yesu, Mwana wa Daudi, unihurumie!”

48 Watu wengi wakamkemea, wakamwambia akae kimya, lakini yeye akazidi kupaza sauti akisema, “Mwana wa Daudi, unihurumie!”

49 Yesu akasimama na kusema, “Mwiteni.”

Hivyo wakamwita yule mtu kipofu wakamwambia, “Jipe moyo! Inuka, anakuita.”

50 Akiwa analivua lile joho lake, alisimama na kumwendea Yesu.

51 Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?”

Yule kipofu akajibu, “Mwalimu, nataka kuona.”

52 Yesu akamwambia, “Nenda zako, imani yako imekuponya.” Mara akapata kuona, akamfuata Yesu njiani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/10-ad18ee103ff7a732e1668087d6d415de.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

seven + 16 =