Marko 11

Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Shangwe

1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni, Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake,

2 akiwaambia, “Nendeni kwenye kijiji kilichoko mbele yenu na mara mwingiapo kijijini, mtakuta mwana punda amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote. Mfungueni, mkamlete hapa.

3 Kama mtu ye yote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”

4 Wakaenda, wakamkuta mwana punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba.

5 Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Mna maana gani mnapomfungua huyo mwana punda?”

6 Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu.

7 Kisha wakamleta huyo mwana punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda.

8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani.

9 Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,

# “Hosana!”

“Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana!

10 “Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”

“Hosana kwake yeye aliye juu!”

11 Yesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwemo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.

Yesu Alaani Mtini Usiozaa

12 Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa.

13 Alipouona mtini kwa mbali, akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini.

14 Yesu akauambia ule mti, “Tangu leo mtu ye yote na asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.

Yesu Atakasa Hekalu

15 Walipofika Yerusalemu, Yesu akaingia Hekaluni akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wananunua na kuuza humo ndani. Akapindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha na viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa,

16 wala hakumruhusu mtu ye yote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu.

17 Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa:

“ ‘Nyumba yangu itaitwa

nyumba ya sala kwa mataifa yote’?

Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyang’anyi.’ ”

18 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumwua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote wa watu walikuwa wanashangazwa na mafundisho yake.

19 Ilipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.

Mtini Ulionyauka

20 Asubuhi yake, walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake.

21 Petro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”

22 Yesu akawajibu akawaambia, “Mwaminini Mungu.

23 Amin, amin nawaambia, mtu ye yote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng’oka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.

24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea nayo yatakuwa yenu.

25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni, mkiwa na neno na mtu ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.

26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.”

Wauliza Kuhusu Mamlaka Ya Yesu

27 Wakafika tena Yerusalemu, wakati Yesu akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamjia.

28 Wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Naye ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”

29 Yesu akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaeleza ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.

30 Niambieni, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

31 Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’

32 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’…” (Waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yohana alikuwa nabii kweli kweli.)

33 Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatujui.”

Naye Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/11-6f63ade6f661027e9f142c452ec6d12a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

seven + four =