Marko 2

Yesu Amponya Mtu Aliyepooza

1 Baada ya siku kadhaa Yesu alirudi Kapernaumu, watu wakasikia kwamba amerudi nyumbani.

2 Hivyo watu wengi wakakusanyika kiasi kwamba hapakubaki nafasi yo yote hata mlangoni! Naye akawahubiria Neno.

3 Ndipo baadhi ya watu wakaja wakamletea Yesu mtu aliyepooza, akiwa amebebwa na watu wanne.

4 Kwa kuwa walikuwa hawawezi kumfikisha kwa Yesu kwa ajili ya umati wa watu, walitoboa tundu kwenye paa mahali pale alipokuwa Yesu, wakamshusha yule aliyepooza kwa kitanda alichokuwa amelalia.

5 Yesu alipoona imani yao, alimwambia yule aliyepooza, “Mwanangu, dhambi zako zimesamehewa.”

6 Basi baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wameketi huko wakawaza mioyoni mwao,

7 “Kwa nini mtu huyu anasema hivi? Huyu anakufuru! Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

8 Mara moja Yesu akatambua kile walichokuwa wanawaza mioyoni mwao, naye akawaambia, “Kwa nini mnawaza hivyo mioyoni mwenu?

9 Ni jambo gani lililo rahisi, kumwambia huyu aliyepooza, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uchukue kitanda chako uende’?

10 Lakini ili mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anao uwezo duniani wa kusamehe dhambi…” Yesu akamwambia yule aliyepooza,

11 “Nakuambia, inuka, chukua kitanda chako uende nyumbani kwako.”

12 Yule mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akachukua kitanda chake akatembea machoni pao wote! Jambo hili likawashangaza wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, “Hatujapata kuona jambo kama hili kamwe!”

Yesu Amwita Lawi (Mathayo)

13 Yesu akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akaanza kuwafundisha.

14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kukusanya kodi, akamwambia, “Nifuate.” Lawi akaondoka, akamfuata Yesu.

15 Yesu alipokuwa akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi pamoja na wenye dhambi walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakimfuata.

16 Baadhi ya walimu wa sheria na Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawauliza wanafunzi wake, “Mbona Yesu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”

17 Yesu aliposikia haya akawaambia, “Walio wazima hawahitaji tabibu, bali wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

Yesu Aulizwa Kuhusu Kufunga

18 Basi wanafunzi wa Yohana pamoja na Mafarisayo walikuwa wakifunga. Baadhi ya watu wakamjia Yesu na kumwuliza, “Mbona wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo hufunga lakini wanafunzi wako hawafungi?”

19 Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kufunga wakati bwana arusi akiwa pamoja nao? Maadamu bwana arusi yuko pamoja nao, hawawezi kufunga.

20 Lakini wakati utakuja ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, siku hiyo ndipo watakapofunga.

21 “Hakuna mtu ashoneaye kiraka cha nguo mpya kwenye nguo iliyochakaa. Akifanya hivyo, kile kiraka kipya kilichoshonewa kwenye nguo iliyochakaa huondoka, nayo ile nguo huchanika zaidi.

22 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, ile divai mpya itavipasua hivyo viriba, kwa hiyo divai itamwagika na viriba vitaharibika. Divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya.”

Bwana Wa Sabato

23 Siku moja ya Sabato, Yesu pamoja na wanafunzi wake, walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakipita wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.

24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo ambalo si halali kufanywa siku ya Sabato?”

25 Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma kamwe alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walipokuwa na njaa na uhitaji wa chakula?

26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu wakati Abiathari akiwa Kuhani Mkuu, akaila ile Mikate Mitakatifu, ambayo ilikuwa hairuhusiwi mtu ye yote kuila isipokuwa makuhani, naye akawapa wenzake.”

27 Kisha Yesu akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.

28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/2-133c114d435642dbff0d57776d3d79a6.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty − sixteen =