Marko 3

Yesu Amponya Mtu Mwenye Mkono Uliopooza

1 Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi na huko palikuwa na mtu mwenye mkono uliopooza.

2 Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki.

3 Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele.”

4 Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato, kufanya jema au baya, kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.

5 Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukapona kabisa!

6 Kisha Mafarisayo wakatoka nje, mara wakaanza kufanya shauri la kumwua Yesu wakiwa na kundi la wafuasi wa Herode.

Umati Wa Watu Wamfuata Yesu

7 Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata.

8 Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, Ng’ambo ya Yordani pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni.

9 Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga.

10 Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa.

11 Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

12 Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.

Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili

13 Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia.

14 Akawachagua kumi na wawili ambao pia aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye na kuwatuma kwenda kuhubiri

15 na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu.

16 Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro),

17 Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo),

18 Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomasi, Yakobo, mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo na

19 Yuda Iskariote, ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Yesu Na Beelzebuli

20 Ndipo Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula.

21 Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”

22 Walimu wa sheria waliotelemka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli! Kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu, anatoa pepo wachafu.”

23 Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani?

24 Kama ufalme ukigawanyika wenyewe kwa wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama.

25 Nayo nyumba kama ikigawanyika yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama.

26 Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe akiwa amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia.

27 Hakuna mtu ye yote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu, ndipo awezapo kuteka nyara.

28 Amin, amin nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa.

29 Lakini ye yote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

30 Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

Mama Na Ndugu Zake Yesu

31 Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita.

32 Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

33 Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”

34 Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama zangu na ndugu zangu.

35 Mtu ye yote anayetenda mapenzi ya Mungu huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/3-69d5e075b3d87913941228fcda2cdb33.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 × 4 =