Marko 4

Mfano Wa Mpanzi

1 Yesu akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Umati wa watu uliokuwa umemkusanyikia na kumzunguka ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ilimbidi Yesu aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo.

2 Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema:

3 “Sikilizeni! Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.

4 Alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka kando ya njia, ndege wakaja na wakazila.

5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba,

6 jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake ilikuwa haina kina.

7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, miiba hiyo ikakua ikaisonga hiyo mimea hivyo haikutoa mazao.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja thelathini, nyingine sitini na nyingine mia moja.”

9 Kisha Yesu akasema, “Mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

Sababu Za Mifano

10 Alipokuwa peke yake, wale waliokuwepo pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili, wakamwuliza kuhusu mifano yake.

11 Naye akawaambia, “Ninyi mmepewa kujua siri ya Ufalme wa Mungu, lakini kwa wale walioko nje, kila kitu husemwa kwao kwa mifano

12 ili,

“ ‘daima waone lakini wasitambue,

daima wasikie lakini wasielewe;

wasije wakageuka, wakatubu na kusamehewa!’ ”

Yesu Afafanua Maana Ya Mfano Wa Mbegu

13 Kisha Yesu akawauliza, “Hamwelewi maana ya mfano huu? Basi mtaelewaje mifano mingine?

14 Yule mpanzi hupanda neno.

15 Hawa ndio wale walio kando ya njia, ambako neno lilipandwa. Walisikiapo neno, Shetani huja mara na kulichukua lile neno lililopandwa ndani yao.

16 Nazo hizi ni zile mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye miamba, wanapolisikia neno, mara hulipokea kwa furaha.

17 Basi kwa kuwa hawana mizizi, hudumu kwa muda mfupi tu, kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, wao mara huiacha imani.

18 Lakini wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye miiba, hulisikia lile neno,

19 lakini masumbufu ya maisha haya, udanganyifu wa mali na tamaa ya mambo mengine huja na kulisonga lile neno na kulifanya lisizae.

20 Wengine, kama mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri, hulisikia lile neno, wakalipokea na kutoa mazao: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mara mia moja ya ile iliyopandwa.”

Mfano Wa Taa

21 Akawaambia, “Je, taa huwashwa na kufunikwa chini ya kikapu au mvunguni mwa kitanda? Je, haiwashwi na kuwekwa juu ya kinara chake?

22 Kwa kuwa hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna jambo lo lote la siri ambalo halitaletwa nuruni.

23 Mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

24 Naye akawaambia, “Iweni waangalifu na yale mnayosikia. Kipimo mnachotumia kuwapimia wengine, ndicho kitakachotumika kuwapimia ninyi, hata na zaidi.

25 Kwa maana aliye na kitu ataongezewa na yeye asiye na kitu hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”

Mfano Wa Mbegu Inayoota

26 Pia akawaambia, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu apandaye mbegu shambani.

27 Akiisha kuzipanda, usiku na mchana, akiwa amelala au ameamka, mbegu huota na kukua pasipo yeye kujua ikuavyo.

28 Udongo huifanya iote kuwa mche, halafu suke, kisha nafaka kamili kwenye suke.

29 Lakini nafaka inapokuwa imekomaa, mara mkulima huingia shambani na mundu wa kuvunia maana mavuno yamekuwa tayari.”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

30 Akawaambia tena, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Au tutumie mfano gani ili kuueleza?

31 Uko kama punje ya haradali, ambayo ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote zinazopandwa ardhini.

32 Lakini ikishaota, hukua ikawa mmea mkubwa kuliko yote katika bustani, ikawa na matawi makubwa hata ndege wa angani kujenga viota kwenye matawi yake.”

33 Kwa mifano mingine mingi kama hii Yesu alinena nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulielewa.

34 Hakusema nao neno lo lote pasipo mifano. Lakini alipokuwa na wanafunzi wake, aliwafafanulia kila kitu.

Yesu Atuliza Dhoruba

35 Siku hiyo, ilipokaribia jioni, aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke na twende mpaka ng’ambo.”

36 Wakiuacha ule umati wa watu nyuma, wakamchukua vile vile kama alivyokuwa kwenye mashua. Palikuwa pia na mashua nyingine nyingi pamoja naye.

37 Kukawa na dhoruba kali, nayo mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikawa karibu kujaa maji.

38 Wanafunzi wake wakamwamsha, wakamwambia, “Mwalimu, hujali kama tunazama?”

39 Akaamka, akaukemea ule upepo, akayaambia yale mawimbi, “Uwe kimya! Tulia!” Ule upepo ukatulia, kukawa shwari kabisa.

40 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kwa nini mnaogopa hivyo? Je, bado hamna imani?”

41 Nao wakawa wameogopa sana, wakaulizana, “Ni nani huyu ambaye hata upepo na mawimbi vinamtii?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MRK/4-74f4defb3384b67a4beb90520b4a556b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

3 + eighteen =