Matendo 1

Ahadi Ya Roho Mtakatifu

1 Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo,

2 hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maelekezo kwa njia Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.

3 Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu.

4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke humu Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake.

5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku hizi chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Kupaa Kwa Yesu Kwenda Mbinguni

6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamwuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”

7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.

8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”

9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.

10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao,

11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”

Mathiya Achaguliwa Badala Ya Yuda

12 Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabatokutoka mjini.

13 Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomasi, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelotena Yuda mwana wa Yakobo.

14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwapo wanawake kadha wa kadha na Maria mama yake Yesu pamoja na ndugu zake Yesu.

15 Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema,

16 “Ndugu zangu, ilibidi maandiko yatimie yale ambayo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu.

17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”

18 (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje.

19 Kila mtu huko Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu).

20 “Kama vile ilivyoandikwa katika kitabu cha Zaburi,

“ ‘Mahali pake na pawe ukiwa

wala asiwepo mtu atakayekaa humo,’

na,

“ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake.’

21 Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipoingia na kutoka katikati yenu,

22 kuanzia ubatizo wa Yohana mpaka siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”

23 Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yosefu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya.

24 Kisha wakaomba, wakasema, “Bwana, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua

25 ili achukue nafasi ya huduma ya utume ambayo Yuda aliiacha ili aende mahali pake mwenyewe.”

26 Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/1-8e9dd28394e8feb14284adf386bc0772.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 + 3 =