Matendo 2

Kushuka Kwa Roho Mtakatifu

1 Ilipowadia siku ya Pentekoste, walikuwa wote mahali pamoja.

2 Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliotoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi.

3 Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.

5 Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu.

6 Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7 Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya?

8 Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa?

9 Warparthi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia,

10 Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi,

11 Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.”

12 Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”

13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa mvinyo!”

Petro Ahutubia Umati

14 Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na moja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize.

15 Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi!

16 Hawa hawakulewa, ila jambo hili ni lile lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:

17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Bwana,

nitamimina Roho wangu

juu ya wote wenye mwili.

Wana wenu na binti zetu watatabiri,

vijana wenu wataona maono

na wazee wenu wataota ndoto.

18 Hata juu ya watumishi wangu

nitamwaga Roho wangu,

nao watatabiri.

19 Nami nitaonyesha maajabu mbinguni juu

na ishara duniani chini, damu,

moto na mvuke wa moshi mnene.

20 Jua litakuwa giza

na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,

kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana

iliyo tukufu.

21 Lakini ye yote atakayeliita

jina la Bwana, ataokolewa.’

22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kwa kupitia yeye, kama ninyi wenyewe mjuavyo.

23 Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimwua kwa kumgongomea msalabani.

24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti.

25 Kwa maana Daudi asema kumhusu yeye:

“ ‘Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote.

Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

sitatikisika.

26 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia

na ulimi wangu unashangilia;

mwili wangu nao utaishi kwa tumaini.

27 Kwa maana hutaniacha kaburini,

wala hutamwacha

aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.

28 Umenionyesha njia za uzima,

utanijaza na furaha mbele zako.’

29 “Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa mpaka leo.

30 Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha enzi.

31 Daudi akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo, kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu.

32 Mungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo.

33 Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia.

34 Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,

“ ‘BWANA alimwambia Bwana wangu:

“Keti upande wangu wa kuume,

35 hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako.” ’

36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulibisha, kuwa Bwana na Kristo.”

Ongezeko La Waamini

37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”

38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu na kwa wale wote walio mbali na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”

40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.”

41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.

Ushirika Wa Waamini

42 Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali.

43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume.

44 Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika.

45 Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, wakamgawia kila mtu kwa kadiri alivyokuwa anahitaji.

46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe,

47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa kwa wale watu waliokuwa wakiokolewa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/2-2b6fb0358cf2443c674797b766e0a22c.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × one =