Matendo 15

Baraza Huko Yerusalemu

1 Baadhi ya watu wakashuka Antiokia kutoka Uyahudi, nao wakawa wanawafundisha ndugu walioamini kwamba, “Isipokuwa mmetahiriwa kufuatana na desturi aliyofundisha Mose, hamwezi kuokoka.”

2 Baada ya Paulo na Barnaba kutokukubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kuingia Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee.

3 Hivyo wakasafirishwa na kanisa, wakiwa njiani wakapitia Samaria wakawaeleza jinsi watu Mataifa walivyoongoka. Habari hizi zikaleta furaha kubwa kwa ndugu wote.

4 Walipofika Yerusalemu, walipokelewa na kanisa na mitume pamoja na wazee, ndipo Paulo na Barnaba wakawaarifu kila kitu Mungu alichokuwa amefanya pamoja nao.

5 Ndipo baadhi ya walioamini wa madhehebu ya Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hao watu Mataifa lazima watahiriwe na waagizwe kuzitii sheria za Mose.”

6 Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili.

7 Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu Mataifa wapate kusikia ujumbe wa injili na kuamini.

8 Mungu, yeye ajuaye mioyo, alionyesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama vile alivyotupa sisi.

9 Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani.

10 Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka kongwa shingoni mwa wanafunzi ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba?

11 Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu Kristo, kama wao wanavyookolewa.”

12 Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu Mataifa.

13 Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni.

14 Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonyesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka katika watu Mataifa kwa ajili ya Jina lake.

15 Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:

16 “ ‘Baada ya mambo haya nitarudi,

nami nitajenga upya

nyumba ya Daudi iliyoanguka.

Nitajenga tena magofu yake

na kuisimamisha,

17 ili wanadamu wengine wote

wapate kumtafuta Bwana,

hata wale watu Mataifa wote

ambao wanaitwa kwa Jina langu,

asema Bwana, afanyaye mambo haya’

18 ambayo yamejulikana tangu zamani.

19 “Kwa hiyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwasumbue watu Mataifa wanaomgeukia Mungu kwa desturi zetu,

20 badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe tu na vitu vilivyotiwa unajisi na uasherati na wasile nyama za wanyama walionyongwa au kunywa damu.

21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”

Barua Kwa Watu Mataifa Waaminio

22 Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao wenyewe na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili ambao walikuwa viongozi miongoni mwa ndugu.

23 Wakatumwa na barua ifuatayo:

Sisi mitume na wazee, ndugu zenu,

Kwa ndugu Mataifa mlioamini mlioko Antiokia, Shamu na Kilikia:

Salamu.

24 Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiwataabisha mawazo yenu.

25 Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,

26 watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo.

27 Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia.

28 Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wo wote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima:

29 Kwamba mjiepushe na kitu cho chote kilichotolewa sadaka kwa sanamu, kunywa damu, nyama ya wanyama walionyongwa na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya mtakuwa mmefanya vyema.

Kwaherini.

30 Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua.

31 Nao hao watu wakiisha kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo.

32 Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga katika imani wale ndugu walioamini.

33 Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma.

34 [Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.]

35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi waliwafundisha na kuhubiri neno la Bwana.

SAFARI YA PILI YA PAULO YA KITUME (15:41–18:22)

Paulo Na Barnaba Wagawanyika

36 Baada ya siku kadhaa, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote ambamo tulihubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.”

37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye.

38 Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi nao.

39 Pakatokea kutokukubaliana kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro.

40 Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana.

41 Akapitia Shamu na Kilikia, akiimarisha makanisa ya huko.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/15-c0379c3f6e22eca653595eb16801ced6.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 × three =