Matendo 16

Timotheo Aungana Na Paulo Na Sila

1 Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani.

2 Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio

3 Paulo alitaka Timotheo afuatane naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwa wanaishi eneo lile kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani.

4 Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa yale maamuzi yaliyokuwa yametolewa.

5 Hivyo makanisa yakawa imara katika imani na kuongezeka kiidadi kila siku.

6 Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, wakiwa wamekatazwa na Roho Mtakatifu wasihubiri neno huko Asia.

7 Walipofika kwenye mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.

8 Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa.

9 Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia ukatusaidie.”

10 Baada ya Paulo kuona maono haya, mara tulijiandaa kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kwa hakika kwamba Mungu ametuita kuhubiri habari njema huko.

Kuongoka Kwa Lidia

11 Tukasafiri kwa njia ya bahari kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, kesho yake tukafika Neapoli.

12 Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa Makedonia sehemu walipokuwa wanakaa Warumi, nasi tukakaa kwenye mji huo kwa siku kadhaa.

13 Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko.

14 Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanya biashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo.

15 Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumbani mwake, alitukaribisha nyumbani mwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.

Paulo Na Sila Watiwa Gerezani

16 Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusalia, tulikutana na mtumwa mmoja wa kike ambaye alikuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapatia mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri.

17 Huyu mtumwa wa kike alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.”

18 Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile.

19 Basi mabwana wa yule mtumwa wa kike walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta mpaka sokoni mbele ya viongozi wa mji.

20 Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi.

21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Kirumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”

22 Umati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko.

23 Baada ya kuchapwa sana wakatupwa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu,

24 kwa kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani na akawafunga miguu yao kwa minyororo.

25 Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

26 Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka.

27 Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka.

28 Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”

29 Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila.

30 Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini ili nipate kuokoka?”

31 Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na wa nyumbani mwako.”

32 Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake.

33 Wakati ule ule yule mkuu wa gereza akawachukua akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa.

34 Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia meza mbele yao, yeye pamoja na wa nyumbani mwake wote wakafurahi sana kwa kuwa amemwamini Mungu.

35 Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waache waende zao.”

36 Mkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaache huru, kwa hiyo tokeni.”

37 Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raia wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”

38 Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raia wa Rumi.

39 Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji.

40 Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walikwenda nyumbani kwa Lidia, ambapo walikutana na wale ndugu walioamini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/16-0cec2393049e2d3d913162ac52be00c6.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

19 + ten =