Matendo 4

Petro Na Yohana Mbele Ya Baraza

1 Wakati Petro na Yohana walipokuwa wakisema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masudakayo wakawajia wakiwa

2 wamekasirika sana kwa sababu hao mitume walikuwa wanawafundisha watu na kuhubiri kwamba katika Yesu kuna ufufuo wa wafu.

3 Wakawakamata Petro na Yohana na kuwatia gerezani mpaka kesho yake kwa kuwa ilikuwa jioni.

4 Lakini wengi wale waliosikia lile neno waliamini, idadi yao ilikuwa yapata wanaume 5,000.

5 Siku ya pili yake viongozi wa Kiyahudi, wazee na waandishi wa sheria wakakusanyika Yerusalemu,

6 walikuwepo Kuhani Mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda na wengi wa jamaa ya Kuhani Mkuu.

7 Wakiisha kuwasimamisha Petro na Yohana katikati yao, wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au kwa jina la nani mmefanya jambo hili?”

8 Petro akiwa amejaa Roho Mtakatifu akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu,

9 kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa,

10 ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa uwezo wa Yesu, kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa.

11 Huyu Yesu ndiye

“ ‘lile jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa,

ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’

12 Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna Jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Ujasiri Wa Petro Na Yohana Washangaza Watu

13 Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu.

14 Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lo lote kuwapinga.

15 Wakawaamuru watoke nje ya barazawakati wakisemezana jambo hilo wao kwa wao.

16 Wakaulizana, “Tuwafanyie nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha mwujiza huu mkubwa walioufanya ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu.

17 Lakini ili kuzuia jambo hili lisiendelee kuenea zaidi miongoni mwa watu, ni lazima tuwaonye watu hawa ili wasiseme tena na mtu ye yote kwa jina la Yesu.”

18 Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu.

Imetupasa Kumtii Mungu Kuliko Wanadamu

19 Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko Mungu.

20 Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”

21 Baada ya vitisho vingi, wakawaacha waende zao. Hawakuona njia yo yote ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu, kwa kuwa watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetukia.

22 Kwa kuwa umri wa yule mtu aliyekuwa ameponywa kwa mwujiza ulikuwa zaidi ya miaka arobaini.

Maombi Ya Waamini

23 Mara Petro na Yohana walipoachiwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.

24 Watu hao waliposikia hayo, wakainua sauti zao wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mwenyezi, uliyeumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo.

25 Wewe ulisema kwa Roho Mtakatifu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema:

“ ‘Mbona watu Mataifa wanaghadhibika,

na kabila za watu zinawaza ubatili?

26 Wafalme wa dunia wamejipanga

na watawala wanakusanyika pamoja

dhidi ya Bwana

# na dhidi ya Mpakwa Mafutawake.’

27 Ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na watu Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu dhidi ya mwanao mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta.

28 Wao wakafanya yale ambayo uweza wako na mapenzi yako yalikuwa yamekusudia yatokee tangu zamani.

29 Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu.

30 Nyosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.”

31 Walipokwisha kuomba, mahali pale walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

Walioamini Washirikiana Mali Zao

32 Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema cho chote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho.

33 Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote.

34 Wala hapakuwepo mtu ye yote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa,

35 wakaiweka miguuni pa wale mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

36 Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja),

37 aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/4-01d250ef26d7dbdb206cc05e0e5fa862.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × two =