Matendo 3

Petro Amponya Mlemavu Kwa Jina La Yesu

1 Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri.

2 Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni.

3 Huyu mtu akiwaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, aliwaomba wampe sadaka.

4 Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.”

5 Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

6 Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu wa Nazareti simama, uende.”

7 Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu.

8 Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu.

9 Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu,

10 wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.

Petro Anashuhudia Kuwa Yesu Anaponya

11 Yule mtu kiwete aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wanawakimbilia mpaka kwenye ukumbi wa Solomoni.

12 Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi waume wa Israeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumefanya mtu huyu kutembea?

13 Mungu wa Abrahamu na Isaki na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Yesu ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake.

14 Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule mwuaji.

15 Hivyo mkamwua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya.

16 Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni kwa jina la Yesu na imani ile itokayo kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama ninyi wote mnavyoona.

17 “Sasa ndugu zangu, najua ya kuwa ninyi mlitenda bila kujua, kama walivyofanya viongozi wenu.

18 Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Kristoatateswa.

19 Tubuni basi mkamgeukie Mungu, ili dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana.

20 Kwamba apate kumtuma Kristo, ambaye amewekwa kwa ajili yenu, yaani Yesu,

21 ambaye ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyosema kwa vinywa vya manabii wake wote watakatifu kabla ya mwanzo wa ulimwengu.

22 Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu, itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia.

23 Mtu ye yote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atakatiliwa mbali kabisa na watu wake.’

24 “Naam, manabii wote tangu Samweli na wale waliofuata baada yake, wote walionena walitabiri kuhusu siku hizi.

25 Ninyi ndio wana wa manabii na wa Agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Abrahamu, ‘Katika wewe, jamaa zote za duniani watabarikiwa.’

26 Mungu alipomfufua Yesu Mwanawe, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu kutoka katika njia yake mbaya.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/3-0f84bfa9e771c51cdc8bf1d043ce71fb.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × 4 =