Matendo 7

Hotuba ya Stefano

1 Ndipo Kuhani Mkuu akamwuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?”

2 Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani,

3 akamwambia, ‘Ondoka katika nchi yako na kutoka kwa jamii yako uende katika nchi nitakayokuonyesha.’

4 “Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa.

5 Mungu hakumpa urithi wo wote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Abrahamu hakuwa na mtoto.

6 Mungu akasema naye hivi, ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kutendewa vibaya miaka 400.’

7 Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa na baadaye watatoka katika nchi hiyo na kuniabudu mahali hapa.’

8 Ndipo akampa Abrahamu Agano la tohara. Naye Abrahamu akamzaa Isaki na kumtahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa kwake. Baadaye Isaki akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale wazee wetu wakuu kumi na wawili.

9 “Kwa sababu wazee wetu wakuu walimwonea wivu Yosefu ndugu yao, walimwuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye.

10 Akamwokoa kutoka katika mateso yote yaliyompata, tena akampa kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimweka kuwa mtawala juu ya Misri na juu ya jumba lote la kifalme.

11 “Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula.

12 Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza.

13 Walipokwenda mara ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, nao ndugu zake Yosefu wakajulishwa kwa Farao.

14 Ndipo Yosefu akatuma wamlete Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote, jumla yao walikuwa watu sabini na watano.

15 Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia.

16 Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.

17 “Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Abrahamu, watu wetu walizidi na kuongezeka sana.

18 Ndipo mfalme mwingine ambaye hakujua lo lote kuhusu Yosefu, akatawala Misri.

19 Huyu mfalme akawatendea watu wetu kwa hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe.

20 “Wakati huo Mose alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani kwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu.

21 Waliposhindwa kumficha zaidi, wakamweka nje mtoni na binti Farao akamchukua akamtunza kama mtoto wake mwenyewe.

22 Mose akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo.

23 “Mose alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli.

24 Aliona mmoja wao akionewa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamwua kulipiza kisasi.

25 Mose alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa.

26 Siku iliyofuata Mose aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kuumizana?’

27 “Lakini yule mtu aliyekuwa akimwonea mwenzake akamsukuma Mose kando, akamwuliza, ‘Ni nani alikuweka uwe mtawala na mwamuzi juu yetu?

28 Je, unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri jana?’

29 Mose aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume.

30 “Basi baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Mose jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto.

31 Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Bwana, ikisema:

32 ‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Yakobo.’ Mose alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama.

33 “Ndipo Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana hapo unaposimama ni mahali patakatifu.

34 Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’

35 “Huyu ndiye Mose yule waliyemkataa wakisema, ‘Ni nani aliyekufanya uwe mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka.

36 Aliwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri, baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamuna katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.

37 “Huyu ndiye yule Mose aliyewaambia Waisraeli, ‘Mungu atawainulia nabii kutoka miongoni mwa ndugu zenu.’

38 Huyu ndiye yule Mose aliyekuwa katika kusanyiko huko jangwani, ambaye malaika alisema naye pamoja na baba zetu kwenye Mlima Sinai, naye akapokea maneno yaliyo hai ili atupatie.

39 “Lakini baba zetu walikataa kumtii Mose, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena.

40 Wakamwambia Aroni, ‘Tufanyie miungu watakaotuongoza, kwa maana mtu huyu Mose aliyetutoa Misri hatujui yaliyompata.’

41 Huu ndio wakati walipotengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichotengeneza kwa mikono yao wenyewe.

42 Ndipo Mungu akageuka, akawaacha waabudu jeshi lote la mbinguni kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii:

“ ‘Je, mlinitolea Mimi dhabihu na sadaka

kwa kipindi cha miaka arobaini kule jangwani, enyi nyumba ya Israeli?

43 La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki

na ya mungu wenu Refani,

vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu.

Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli.

44 “Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani. Lilikuwa limetengenezwa kama Mungu alivyokuwa amemwelekeza Mose, kulingana na kielelezo alichoona.

45 Baba zetu wakiisha kulipokea hema kwa kupokezana wakiongozwa na Yoshua katika milki ya nchi kutoka kwa yale mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao, nalo likadumu katika nchi mpaka wakati wa Daudi,

46 ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.

47 Lakini alikuwa Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.

48 “Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema:

49 “ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi,

na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu.

Mtanijengea nyumba ya namna gani?

asema Bwana.

Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi?

50 Je, mikono yangu haikuumba vitu hivi vyote?’

51 “Ninyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zetu.

52 Je, kuna nabii gani ambaye baba zetu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji.

53 Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”

Stefano Apigwa Mawe

54 Waliposikia haya wakaghadhabika, wakamsagia Stefano meno.

55 Lakini yeye Stefano akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, naye Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu.

56 Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”

57 Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja.

58 Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni mwa kijana mmoja ambaye jina lake aliitwa Sauli.

59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu”

60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/7-7a36112779864a61cb0c06fdae778546.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ten + 9 =