Matendo 8

1 Naye Sauli alikuwepo pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano.

Kanisa Lateswa Na Kutawanyika

Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Uyahudi na Samaria.

2 Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwombolezea sana.

3 Lakini kwa habari ya Sauli alikuwa analiharibu kanisa, akiingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanawake na wanaume na kuwatia gerezani.

Filipo Ahubiri Injili Samaria

4 Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipokwenda.

5 Filipo akatelemkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo.

6 Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema.

7 Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa.

8 Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

Simoni, Mchawi

9 Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu,

10 watu wote wakubwa kwa wadogo wakamsikiliza na kumaka wakisema “Mtu huyu ndiye uweza wa Mungu ujulikanao kama ‘Uweza Mkuu.’ ”

11 Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake.

12 Lakini watu walipomwamini Filipo akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa wanaume na wanawake.

13 Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.

14 Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko.

15 Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu,

16 kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu.

17 Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho Mtakatifu.

18 Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akawapa fedha

19 akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.”

20 Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha!

21 Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.

22 Kwa hiyo tubia huu uovu wako na umwombe Mungu, ili yamkini, aweze kusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako.

23 Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.”

24 Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lo lote lisinitukie.”

25 Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana, wakarudi Yerusalemu wakihubiri injili katika vijiji vingi vya Samaria.

Filipo Na Towashi Wa Kushi

26 Basi Malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara itokayo Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.”

27 Hivyo akaondoka na kwenda. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa amekwenda Yerusalemu ili kuabudu,

28 naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi garini mwake akisoma kitabu cha nabii Isaya.

29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”

30 Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Je, unaelewa hayo usomayo?”

31 Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye.

32 Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la maandiko:

“Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni,

kama mwana-kondoo anyamazavyo

mbele yake yeye amkataye manyoya,

hivyo hakukifungua kinywa chake.

33 Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake.

Nani awezaye kueleza juu ya kizazi chake?

Kwa maana maisha yake yameondolewa

kutoka duniani.”

34 Yule towashi akamwuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena kwa habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?”

35 Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la maandiko akamweleza habari njema za Yesu.

36 Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamwambia Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” (

37 Filipo akamwambia, “Kama ukiamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu).”

38 Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Wakatelemka kwenye maji wote wawili, yule towashi na Filipo, naye Filipo akambatiza.

39 Nao walipopanda kutoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi.

40 Filipo akajikuta yuko Azoto, akasafiri akihubiri injili katika miji yote mpaka alipofika Kaisaria.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ACT/8-ddd1887ef7f7e0da01d9e0e8212f9867.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

16 − five =