Mathayo 13

Mfano Wa Mpanzi

1 Siku iyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba akaketi kando ya bahari.

2 Umati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari.

3 Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.

4 Alipokuwa akipanda, baadhi zikaanguka kando ya njia, ndege wakaja na kuzila.

5 Nyingine zikaanguka sehemu yenye mawe, ambapo hapana udongo mwingi. Zikaota haraka kwa sababu udongo ulikuwa hauna kina.

6 Lakini jua lilipozidi, mimea hiyo ilinyauka na kukauka kwa sababu mizizi yake haikuwa na kina.

7 Mbegu nyingine zilianguka katikati ya miiba, miiba hiyo ikakua ikazisonga.

8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini na nyingine mara thelathini.

9 Yeye mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

Sababu Ya Kufundisha Kwa Mifano

10 Wanafunzi wake wakamwendea wakamwuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”

11 Akawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao sivyo.

12 Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele, lakini yule asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa.

13 Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano:

“Ingawa wanatazama, hawaoni,

wanasikiliza, lakini hawasikii

wala hawaelewi.

14 Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema:

“ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa,

na pia mtatazama lakini hamtaona.

15 Kwa maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito,

hawasikii kwa masikio yao,

na wamefumba macho yao.

Wasije wakaona kwa macho yao,

wakasikia kwa masikio yao,

wakaelewa kwa mioyo yao,

wakageuka, nami nikawaponya.’

16 Lakini heri macho yenu, kwa sababu yanaona na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia.

17 Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona, nao hawakuyaona na kusikia yale mnayosikia lakini hawakuyasikia.

Maelezo Ya Mfano Wa Mbegu

18 “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi:

19 Mtu ye yote anaposikia neno la Ufalme, naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake, hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia.

20 Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na mara hulipokea kwa furaha.

21 Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hukaa kwa muda mfupi. Inapotokea dhiki au mateso kwa ajili ya hilo neno, yeye mara huchukizwa.

22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya dunia na ushawishi wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda.

23 Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika hutoa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”

Mfano Wa Magugu

24 Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.

25 Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea.

27 “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’

28 “Akawajibu, ‘Adui ndiye aliyefanya jambo hili.’

“Wale watumishi wakamwuliza, ‘Je, unataka twende tukayang’oe?’

29 “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyang’oe, kwa maana wakati mking’oa magugu mnaweza mkang’oa na ngano pamoja nayo.

30 Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji, wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto, kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”

Mfano Wa Mbegu Ya Haradali

31 Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua akaipanda shambani mwake.

32 Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hata ndege wa angani huja na kutengeneza viota katika matawi yake.”

Mfano Wa Chachu

33 Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa Mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika vipimo vitatuvya unga mpaka wote ukaumuka.”

Sababu Ya Yesu Kutumia Mifano

34 Yesu alinena mambo haya yote kwa makutano kwa mifano. Wala pasipo mfano hakuwaambia lo lote.

35 Hii ilikuwa ili kutimiza lile lililonenwa kwa vinywa vya manabii kusema:

“Nitakifungua kinywa changu niseme nao kwa mifano,

nitahubiri mambo yaliyofichika

tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.”

Ufafanuzi Wa Mfano Wa Magugu

36 Kisha Yesu akaagana na makutano, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”

37 Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu.

38 Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa Ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu.

39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.

40 “Kama vile magugu yang’olewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia.

41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote.

42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.

43 Ndipo wenye haki watang’aa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

Mfano Wa Hazina Iliyofichwa Na Wa Lulu

44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

45 “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanya biashara aliyekuwa akitafuta lulu safi.

46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

Mfano Wa Wavu

47 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina.

48 Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa.

49 Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki.

50 Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

51 Yesu akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?”

Wakamjibu, “Ndiyo.”

52 Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya Ufalme wa Mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka katika ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”

Yesu Akataliwa Nazareti

53 Yesu alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka.

54 Alipofika mjini kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?”

55 “Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Maria, nao ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda?

56 Nao dada zake wote hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?”

57 Wakachukizwa naye.

Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”

58 Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/13-a919a5133c4e97aa62376d5cfb8e49b5.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

6 − 5 =