Mathayo 14

Yohana Mbatizaji Akatwa Kichwa

1 Wakati huo, Mfalme Herode aliyekuwa mtawala alisikia habari kuhusu sifa za Yesu,

2 akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji, amefufuka kutoka kwa wafu! Hiyo ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”

3 Herode alikuwa amemkamata Yohana akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake,

4 kwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode kwamba, “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.”

5 Herode alitaka sana kumwua Yohana, lakini akaogopa watu kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.

6 Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti wa Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria akamfurahisha sana Herode

7 kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti lo lote atakaloomba.

8 Yeye akiwa amefundishwa na mama yake, huyo binti akasema, “Nipatie kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.”

9 Mfalme akasikitika, lakini kwa ajili ya kile kiapo alichoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake.

10 Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani.

11 Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake.

12 Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu.

Yesu Alisha Watu Elfu Tano

13 Yesu aliposikia haya yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu, kutoka mijini.

14 Yesu alipofika kando ya bahari aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.

15 Ilipofika jioni, wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha, waage makutano ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”

16 Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”

17 Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”

18 Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.”

19 Akaagiza makutano wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate, kisha akawapa wanafunzi wake hiyo mikate na hao samaki, wanafunzi wakawagawia makutano.

20 Wote wakala, wakatosheka, nao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

21 Idadi ya wale watu waliokula walikuwa wanaume 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

Yesu Atembea Juu Ya Maji

22 Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye chombo watangulie kwenda ng’ambo ya pili ya bahari, wakati yeye anawaaga wale makutano.

23 Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake.

24 Wakati huo kile chombo kilikuwa kimeshafika mbali kutoka nchi kavu kikisukwasukwa na mawimbi kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.

25 Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji.

26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.

27 Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni Mimi. Msiogope.”

28 Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”

29 Yesu akamwambia, “Njoo.”

Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu.

30 Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!”

31 Mara Yesu akanyosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”

32 Nao walipoingia ndani ya chombo, upepo ukakoma.

33 Ndipo wote waliokuwamo ndani ya kile chombo wakamwabudu Yesu wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

Yesu Awaponya Wagonjwa Genesareti

34 Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti.

35 Watu wa eneo lile walipomtambua Yesu, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote

36 wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/14-fdea054a7ab78ed9f9ee0c53c4be9752.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eighteen − 9 =