Mathayo 16

Mafarisayo Wadai Ishara

1 Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

2 Akawajibu akawaambia, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu,’

3 nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati.

4 Kizazi cha waovu na cha zinaa hutafuta ishara ya majira, lakini hakitapewa ishara yo yote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake.

Chachu Ya Mafarisayo Na Masadukayo

5 Wanafunzi wake walipofika ng’ambo ya pili ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate.

6 Yesu akawaambia, “Jihadharini, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”

7 Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”

8 Yesu, akitambua mazungumzo yao, akasema, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate?

9 Je, bado tu hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano iliyolisha watu 5,000 na ni idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?

10 Au ile mikate saba iliyolisha watu 4,000 na ni idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya?

11 Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”

12 Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

Petro Amkiri Yesu Kuwa Ni Mwana Wa Mungu

13 Basi Yesu alipofika katika eneo la Kaisaria Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”

14 Wakamjibu, “Baadhi ya watu husema ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya na bado wengine husema, ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”

15 Akawauliza, “Je, ninyi, mnasema mimi ni nani?”

16 Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”

17 Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni.

18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya kuzimu hayataweza kulishinda.

19 Nitakupa funguo za Ufalme wa Mbinguni na lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, lo lote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa Mbinguni.”

20 Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote kwamba yeye ndiye Kristo.

Yesu Anatabiri Juu Ya Kifo Chake

21 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi kwa mikono ya wazee, wakuu wa makuhani na walimu wa sheria na kwamba itampasa auawe na siku ya tatu atafufuka.

22 Petro akamchukua kando akaanza kumkemea, akisema, “Mungu apishie hayo mbali! Jambo hili kamwe halitakupata!”

23 Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

24 Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe na auchukue msalaba wake, anifuate.

25 Kwa maana ye yote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini ye yote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.

26 Kwa maana itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya maisha yake?

27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

28 Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/16-a89bc161473fc620baa899bc75068651.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × 2 =