Mathayo 17

Yesu Abadilika Sura Mlimani

1 Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, na kuwaleta mpaka juu ya mlima mrefu mahali pasipo na watu.

2 Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang’aa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho.

3 Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu.

4 Ndipo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”

5 Petro alipokuwa angali ananena, ghafula, wingu linalong’aa likawafunika na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye sana, msikilizeni yeye.”

6 Wale wanafunzi, waliposikia haya, wakaanguka chini kifudifudi, wakajawa na hofu.

7 Lakini Yesu akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.”

8 Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine ye yote isipokuwa Yesu.

9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, “Msimwambie mtu ye yote maono haya mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka kwa wafu.”

10 Wale wanafunzi wakamwuliza, “Kwa nini basi walimu wa sheria wanasema kwamba lazima Eliya aje kwanza?”

11 Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya lazima aje kwanza naye atatengeneza mambo yote.

12 Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.”

13 Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yohana Mbatizaji.

Yesu Amponya Kijana Mwenye Pepo

14 Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema,

15 “Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji.

16 Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.”

17 Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi hata lini, nami nitawavumilia hadi lini? Mleteni kijana hapa kwangu.”

18 Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

19 Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakati ambapo hakuna watu, wakamwuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani kama punje ndogo ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu.”

21 “Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.”

22 Siku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu.

23 Nao watamwua na siku ya tatu atafufuka.” Wanafunzi wakahuzunika sana.

Yesu Na Petro Watoa Kodi Ya Hekalu

24 Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekaluwakamjia Petro na kumwuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamwuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa.

27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua, fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/17-92d7539442a4741528d3ef4c6aefd5b9.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × 5 =