Mathayo 2

Wataalamu Wa Nyota Wafika Kumwona Mtoto Yesu

1 Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu

2 wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”

3 Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu.

4 Herode akawaita pamoja makuhani wakuu na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristoangezaliwa.

5 Nao wakamwambia, “Katika Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:

6 “ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,

wewe si mdogo miongoni

mwa watawala wa Yuda,

kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala

atakayekuwa mchungaji

wa watu wangu Israeli.’ ”

7 Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilipoonekana.

8 Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia, “Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mumwonapo, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.”

9 Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto.

10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno.

11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.

12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.

Yosefu, Maria Na Mtoto Yesu Wakimbilia Misri

13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”

14 Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri

15 ambako walikaa mpaka Herode alipokufa. Hili lilikuwa, ili litimie lile lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii kusema, “Kutoka Misri nilimwita mwanangu.”

16 Herode alipong’amua kwamba wale wataalamu wa nyota wamemshinda kwa akili, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kufuatana na ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota.

17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia.

18 “Sauti ilisikika huko Rama,

kilio cha huzuni na maombolezo makuu,

Raheli akilia kwa ajili ya wanawe,

akikataa kufarijiwa,

kwa sababu hawako tena.”

Kurudi Kutoka Misri

19 Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri

20 na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”

21 Basi Yosefu, akaondoka akamchukua mtoto na mama yake wakaenda mpaka nchi ya Israeli.

22 Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Uyahudi mahali pa Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya,

23 akaenda akaishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia lile neno lililonenwa na manabii, “Ataitwa Mnazarayo.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/2-839b069cf9b58f149c63b36e2cf15c0e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twelve − 2 =