Mathayo 3

Yohana Mbatizaji Atayarisha Njia

1 Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika Nyika ya Uyahudi, akisema,

2 “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni u karibu.”

3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema,

“Sauti ya mtu aliaye huko nyikani,

‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana,

yanyosheni mapito yake.’ ”

4 Basi Yohana alivaa vazi lililotengenezwa kwa singa za ngamia akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake, chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu.

5 Watu walimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani.

6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

7 Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia, “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?

8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba.

9 Wala msidhani mnaweza kusemezana, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Kwa maana nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka katika mawe haya.

10 Hata sasa shoka limekwisha kuwekwa tayari kwenye mizizi ya mti. Kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.

11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwaRoho Mtakatifu na kwa moto.

12 Chombo chake cha kupuria kiko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, akiikusanya ngano yake ghalani na kuyachoma makapi kwa moto usiozimika.”

Yesu Abatizwa

13 Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize.

14 Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”

15 Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.

16 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikamfungukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake.

17 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/3-381e1740155446a1f04bd88e8865bf67.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 + 9 =