Mathayo 5

Sifa Za Aliyebarikiwa

1 Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia.

2 Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:

3 “Heri walio maskini wa roho,

maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.

4 Heri wale wanaohuzunika,

maana hao watafarijiwa.

5 Heri walio wapole,

maana hao watairithi nchi.

6 Heri wenye njaa na kiu ya haki,

maana hao watatoshelezwa.

7 Heri wenye huruma,

maana hao watapata rehema.

8 Heri walio na moyo safi,

maana hao watamwona Mungu.

9 Heri walio wapatanishi,

maana hao wataitwa wana wa Mungu.

10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki,

maana hao Ufalme wa Mbinguni ni wao.

11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu.

12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kuu.

Chumvi Na Nuru

13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu cho chote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika.

15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba.

16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

Kutimiza Sheria

17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Torati au Manabii, sikuja kuondoa bali kutimiza.

18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yo yote kutoka kwenye Torati mpaka kila kitu kiwe kimetimia.

19 Kwa hiyo, ye yote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini ye yote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni.

20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya walimu wa sheria na Mafarisayo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

Kuhusu Hasira

21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue, ye yote atakayeua atapaswa hukumu.’

22 Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote atakayemkasirikia ndugu yake wa kiume au wa kike, atapaswa hukumu. Tena, ye yote atakayemwambia ndugu yake wa kiume au wa kike, ‘Raca’, yaani kumdharau na kumdhihaki, atapaswa kufanyiwa baraza. Lakini ye yote atakayesema ‘Wewe mpumbavu ulaaniwe!’ Atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako,

24 iache sadaka yako hapo, mbele ya madhabahu, uende kwanza ukapatane na ndugu yako wa kiume au wa kike, kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

25 “Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani.

26 Amin, nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa hadi senti ya mwisho.

Kuhusu Uzinzi

27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini’.

28 Lakini mimi nawaambia kwamba, ye yote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

29 Jicho lako la kuume likikufanya utende dhambi, ling’oe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

30 Kama mkono wako wa kuume ukikufanya utende dhambi, ukate uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

Kuhusu Talaka

31 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu ye yote amwachaye mkewe na ampe hati ya talaka.’

32 Lakini mimi nawaambia, ye yote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na ye yote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa azini.

Kuhusu Kuapa

33 “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’

34 Lakini mimi nawaambia, Msiape kabisa, ama kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu,

35 au kwa nchi, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu, au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu.

36 Nanyi msiape kwa vichwa vyenu kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

37 ‘Ndiyo,’ yenu iwe ‘Ndiyo’ na ‘Hapana’, yenu iwe ‘Hapana.’ Lo lote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.

Kuhusu Kulipiza Kisasi

38 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’

39 Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia,

40 Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua shati lako, mwachie achukue na koti pia.

41 Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili.

42 Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

Upendo Kwa Adui

43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’

44 Lakini mimi ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi,

45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46 Kama mkiwapenda wale wanaowapenda tu, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo?

47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo?

48 Kwa hiyo iweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/5-287f417e0222d2926c445cc3fdde0fa2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

20 − two =