Mathayo 4

Kujaribiwa Kwa Yesu

1 Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kuingia nyikani ili akajaribiwe na ibilisi.

2 Baada ya kufunga siku arobaini mchana na usiku, hatimaye akaona njaa.

3 Mjaribu akamjia na kumwambia, “Kama wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

4 Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa, ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

5 Ndipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na kumweka juu ya mnara mrefu mwembamba wa Hekalu,

6 akamwambia, “Kama wewe ndiye Mwana wa Mungu jitupe chini, kwa kuwa imeandikwa,

“ ‘Atakuagizia malaika zake,

nao watakuchukua mikononi mwao

ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’ ”

7 Yesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

8 Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake,

9 kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”

10 Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako, nawe utamtumikia yeye peke yake.’ ”

11 Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumtumikia.

Yesu Aanza Kuhubiri

12 Yesu aliposikia kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa ametiwa gerezani, alirudi Galilaya.

13 Akaondoka Nazareti akaenda kuishi Kapernaumu mji ulioko karibu na bahari, katika mipaka ya nchi ya Zabuloni na ya Naftali,

14 ili kutimiza unabii wa nabii Isaya, kama alivyosema:

15 “Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali,

kwenye njia ya kuelekea baharini,

ng’ambo ya Yordani,

Galilaya ya watu Mataifa:

16 watu wale waliokaa gizani

wameona nuru kuu

nao wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti,

nuru imewazukia.”

17 Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

Yesu Awaita Wanafunzi Wake Wa Kwanza

18 Wakati Yesu alipokuwa anatembea kando ya Bahari ya Galilaya aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa maana wao walikuwa wavuvi.

19 Yesu akawaambia, “Njoni, nifuateni, nami nitawafanya muwe wavuvi wa watu.”

20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

21 Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo wakiziandaa nyavu zao. Yesu akawaita.

22 Nao mara wakaziacha nyavu zao, pamoja na baba yao, wakamfuata.

Yesu Ahubiri Na Kuponya Wagonjwa

23 Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu, akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu.

24 Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya.

25 Makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Uyahudi na kutoka ng’ambo ya Mto Yordani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/4-f9ac2dfc5a34755fd150da9a30f0b003.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

3 × two =