Mathayo 7

Kuwahukumu Wengine

1 “Usihukumu ili usije ukahukumiwa.

2 Kwa maana kwa jinsi ile unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa na kwa kipimo kile utakachotoa ndicho utakachopokea.

3 “Kwa nini unatazama kibanzi kidogo kilichomo kwenye jicho la ndugu yako na wala huoni boriti iliyoko kwenye jicho lako?

4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe?’

5 Ewe mnafiki, toa kwanza boriti kwenye jicho lako mwenyewe, nawe ndipo utakapoona wazi ili kuondoa kibanzi kilichoko kwenye jicho la ndugu yako.

6 “Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu, wala msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya hivyo, watazikanyaga-kanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.

Omba, Tafuta, Bisha

7 “Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.

8 Kwa maana kila aombaye hupewa, naye atafutaye huona, naye abishaye hufunguliwa mlango.

9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe?

10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka?

11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua jinsi ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao?

12 Kwa hiyo cho chote ambacho mnataka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Torati na Manabii.

Njia Nyembamba Na Njia Pana

13 “Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo.

14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

Mti Na Tunda Lake

15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali.

16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba au tini kwenye michongoma?

17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya.

18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.

19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

20 Hivyo kwa matunda yao mtawatambua.

Mwanafunzi Wa Kweli

21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’

23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

Msikiaji Na Mtendaji

24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba.

25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, lakini haikuanguka kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba.

26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga.

27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

28 Yesu alipomaliza kusema maneno haya, makutano ya watu wakashangazwa sana na mafundisho yake,

29 kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/7-89cc956bb23cb8869ceee4ea0a9cdcbb.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × four =