Mathayo 8

Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma

1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata.

2 Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”

3 Yesu akanyosha mkono wake akamgusa, akamwambia, “Nataka, takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake.

4 Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu ye yote. Lakini nenda, ukajionyeshe kwa kuhani na utoe sadaka aliyoamuru Mose, iwe ushuhuda kwao kwamba umepona.”

Yesu Amponya Mtumishi Wa Jemadari

5 Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada,

6 akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”

7 Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”

8 Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.

9 Kwa kuwa mimi nami niko chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu ‘Nenda,’ huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo’, huja. Nami nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ hufanya.”

10 Yesu aliposikia maneno haya, akashangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, amin nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona imani kubwa namna hii.

11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni.

12 Lakini warithi wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwa na kulia na kusaga meno.”

13 Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.

Yesu Aponya Wengi

14 Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wake Petro amelala kitandani akiwa ana homa.

15 Akamgusa mkono wake na homa ikamtoka, naye akainuka na kuanza kumhudumia.

16 Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuponya wagonjwa wote.

17 Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:

“Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu

na alichukua magonjwa yetu.”

Gharama Ya Kumfuata Yesu

18 Yesu alipoona makutano mengi wamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke mpaka ng’ambo.

19 Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata po pote uendako.”

20 Naye Yesu akamwambia, “Mbweha wana mashimo, nao ndege wa angani wana viota vyao, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

21 Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”

22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, nawe waache wafu wazike wafu wao.”

Yesu Atuliza Dhoruba

23 Naye alipoingia kwenye chombo, wanafunzi wake wakamfuata.

24 Ghafula kukainuka dhoruba kali baharini hata chombo kikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi.

25 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”

26 Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kuu.

27 Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

Wawili Wenye Pepo Waponywa

28 Walipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu wakitoka makaburini walikutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile.

29 Wakapiga kelele, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”

30 Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha.

31 Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu tuende kwenye lile kundi la nguruwe.”

32 Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likatelemka mbio gengeni, likaingia baharini na kufa ndani ya maji.

33 Wale waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote kuhusu yale yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu.

34 Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Yesu. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MAT/8-e8b4ea0652e416d2e3bde5b78855b1dd.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

20 − 14 =