Mhubiri 1

Kila Kitu Ni Ubatili Mtupu

1 Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu:

2 “Ubatili mtupu! Ubatili mtupu!”

Mhubiri anasema.

“Ubatili mtupu!

Kila kitu ni ubatili.”

3 Mwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote

anayotaabikia chini ya jua?

4 Vizazi huja na vizazi hupita,

lakini dunia inadumu milele.

5 Jua huchomoza na jua huzama,

nalo huarakisha kurudi maawioni.

6 Upepo huvuma kuelekea kusini

na kugeukia kaskazini,

hurudia mzunguko huo huo,

daima ukirudia njia yake.

7 Mito yote hutiririka baharini,

hata hivyo bahari kamwe haijai.

Mahali mito inapotoka,

huko hurudi tena.

8 Vitu vyote vinachosha,

zaidi kuliko mtu anavyoweza kusema.

Jicho kamwe halitosheki kutazama,

wala sikio halishibi kusikia.

9 Kile kilichokuwapo kitakuwapo tena,

kile kilichofanyika kitafanyika tena,

hakuna kilicho kipya chini ya jua.

10 Kuna kitu cho chote ambacho mtu anaweza kusema,

“Tazama! Kitu hiki ni kipya”?

Kilikuwapo tangu zamani za kale,

kilikuwapo kabla ya wakati wetu.

11 Hakuna kumbukumbu ya watu wa zamani,

hata na wale ambao hawajaja bado

hawatakumbukwa

na wale watakaofuata baadaye.

Hekima Ni Ubatili

12 Mimi, Mhubiri, nilikuwa mfalme katika Yerusalemu.

13 Nilitumia muda wangu wote kujifunza na kuvumbua kwa hekima yote yanayofanyika chini ya mbingu. Jinsi gani Mungu ameweka mzigo mzito juu ya wanadamu!

14 Nimeshaona mambo yote yanayotendeka chini ya jua, hayo yote ni ubatili, hii ni kukimbiza upepo.

15 Kilichopindika hakiwezekani kunyoshwa,

kile ambacho hakipo haiwezekani kukihesabu.

16 Niliwaza mwenyewe, “Tazama, nimekua na kuongezeka katika hekima kuliko ye yote aliyewahi kutawala Yerusalemu kabla yangu. Nimekuwa na uzoefu mkubwa wa hekima na maarifa.”

17 Ndipo nilipojitahidi kufahamu kutofautisha hekima, wazimu na upumbavu, lakini nikatambua hata hili nalo ni kukimbiza upepo.

18 Kwa kuwa hekima nyingi huleta huzuni kubwa;

maarifa yanapoongezeka, masikitiko yanaongezeka.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ECC/1-cc76df45a6ce50f66cc53b5ad9a9a9e2.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty − 11 =