Mika 7

Taabu Ya Israeli

1 Taabu gani hii niliyo nayo!

Nimefanana na yule akusanyaye

matunda ya kiangazi,

aokotaye masazo baada ya kuvunwa

shamba la mizabibu;

hakuna kishada chenye matunda ya kula,

hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani.

2 Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka katika nchi;

hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki.

Watu wote wanavizia kumwaga damu,

kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu.

3 Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya,

mtawala anadai zawadi,

hakimu anapokea rushwa,

wenye nguvu wanaamuru wanachotaka:

wote wanafanya shauri baya pamoja.

4 Aliye mwema kupita wote kati yao

ni kama mchongoma,

anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao

ni mbaya kuliko uzio wa miiba.

Siku ya walinzi wako imewadia,

siku atakayokutembelea Mungu.

Sasa ni wakati wao

wa kuchanganyikiwa.

5 Usimtumaini jirani;

usiweke matumaini kwa rafiki.

Hata kwa yule alalaye kifuani mwako

uwe mwangalifu kwa maneno yako.

6 Kwa kuwa mwana humdharau baba yake,

naye binti huinuka dhidi ya mama yake,

mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake:

adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.

7 Lakini mimi, namtazamaBwanakwa matumaini,

namngoja Mungu Mwokozi wangu;

Mungu wangu atanisikia mimi.

Israeli Atainuka

8 Usifurahie msiba wangu, Ee adui yangu!

Ingawa nimeanguka, nitainuka.

Japo ninaketi gizani,

Bwanaatakuwa nuru yangu.

9 Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake,

nitabeba ghadhabu yaBwana,

mpaka atakaponitetea shauri langu

na kuithibitisha haki yangu.

Atanileta nje kwenye mwanga,

nami nitaiona haki yake.

10 Kisha adui yangu ataliona

naye atafunikwa na aibu,

yule aliyeniambia,

“Yu wapiBwanaMungu wako?”

Macho yangu yataona kuanguka kwake,

hata sasa atakanyagwa chini ya mguu

kama tope barabarani.

11 Siku ya kujenga kuta zako itawadia,

siku ya kupanua mipaka yako.

12 Siku hiyo watu watakuja kwako

kutoka Ashuru na miji ya Misri,

hata kutoka Misri hadi Eufrati

na kutoka bahari hadi bahari

na kutoka mlima hadi mlima.

13 Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake,

kwa sababu ya matunda ya matendo yao.

Sala Na Sifa

14 Wachunge watu wako kwa fimbo yako,

kundi la urithi wako,

ambalo linaishi peke yake msituni,

katika nchi ya malisho yenye rutuba.

Waache walishe katika Bashani na Gileadi

kama ilivyokuwa siku za kale.

15 “Kama siku zile mlipotoka Misri,

nitawaonyesha maajabu yangu.”

16 Mataifa yataona na kuaibika,

waliondolewa nguvu zao zote.

Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao

na masikio yao yatakuwa na uziwi.

17 Wataramba mavumbi kama nyoka,

kama viumbe vitambaavyo juu ya ardhi.

Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka;

watamgeukiaBwanaMungu wetu kwa hofu

nao watakuogopa.

18 Ni nani Mungu kama wewe,

ambaye anaachilia dhambi

na kusamehe makosa

ya mabaki ya urithi wake?

Wewe huwi na hasira milele,

bali unafurahia kuonyesha rehema.

19 Utatuhurumia tena,

utazikanyaga dhambi zetu

chini ya nyayo zako,

na kutupa maovu yetu yote

katika vilindi vya bahari.

20 Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,

nawe utamwonyesha Abrahamu rehema,

kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu

siku za kale.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/MIC/7-ca45d233b469bf8ef7c59311f5f4c08e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

11 + eleven =