Mithali 17

1 Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu

kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi.

2 Mtumishi mwenye hekima atatawala juu ya mwana aaibishaye,

naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.

3 Kalibu ni kwa ajili ya fedha na tanuru ni kwa ajili ya dhahabu,

baliBwanahuujaribu moyo.

4 Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya,

mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.

5 Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake;

ye yote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.

6 Wana wa wana ni taji la wazee,

nao wazazi ni fahari ya watoto wao.

7 Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu,

ni mibaya kiasi gani midomo ya uongo kwa mtawala!

8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho,

ko kote kigeukiapo, hufanikiwa.

9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo,

bali ye yote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.

10 Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua

kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.

11 Mtu mbaya hupenda kuasi tu,

mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake.

12 Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyang’anywa watoto wake,

kuliko mpumbavu katika upumbavu wake.

13 Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema,

kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.

14 Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji,

kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza.

15 Yeye asemaye asiye na haki ana haki,

naye asemaye mwenye haki hana haki,

Bwanahuwachukia sana wote wawili.

16 Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu,

wakati yeye hana haja ya kupata hekima?

17 Rafiki hupenda wakati wote

naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.

18 Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani

naye huweka dhamana kwa jirani yake.

19 Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi,

# naye ainuaye sana lango lakehutafuta uharibifu.

20 Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa;

naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu

huangukia kwenye taabu.

21 Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni,

hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu.

22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,

bali roho iliyonyong’onyea hukausha mifupa.

23 Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri,

ili kupotosha njia ya haki.

24 Mtu wa ufahamu huitazama hekima,

lakini macho ya mpumbavu huhangaika

hadi kwenye miisho ya dunia.

25 Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake

na uchungu kwa yeye aliyemzaa.

26 Sio vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia,

au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao.

27 Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia,

naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.

28 Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima kama akinyamaza,

na mwenye ufahamu kama akiuzuia ulimi wake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/17-a994f3777eb3a1d41931d0312be762c3.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

two × four =