Mithali 23

1 Uketipo kula chakula na mtawala,

angalia vyema kile kilicho mbele yako,

2 na utie kisu kooni mwako

kama ukiwa mlafi.

3 Usitamani vyakula vyake vitamu

kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.

4 Usijitaabishe ili kuupata utajiri,

uwe na hekima kuonyesha kujizuia.

5 Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,

huwa kama umepata mabawa ghafula,

ukaruka na kutoweka angani kama tai.

6 Usile chakula cha mtu mchoyo,

usitamani vyakula vyake vitamu,

7 kwa maana yeye ni aina ya mtu

ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama.

Anakuambia, “Kula na kunywa,”

lakini moyo wake hauko pamoja nawe.

8 Utatapika kile kidogo ulichokula,

nawe utakuwa umepoteza bure

maneno yako ya kumsifu.

9 Usizungumze na mpumbavu,

kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.

10 Usiondoe jiwe la mpaka wa zamani

wala kujiingiza kwenye mashamba ya yatima,

11 kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu,

atalichukua shauri lao dhidi yako.

12 Elekeza moyo wako kwenye mafundisho

na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.

13 Usimnyime mtoto adhabu,

kwa maana ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.

14 Mwadhibu kwa fimbo

# na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini.

15 Mwanangu, kama moyo wako una hekima,

basi moyo wangu utafurahi,

16 utu wangu wa ndani utafurahi,

wakati midomo yako

itakapozungumza lililo sawa.

17 Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi,

bali kila mara uwe na bidii katika kumchaBwana.

18 Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako,

nalo taraja lako halitakatiliwa mbali.

19 Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima,

weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.

20 Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,

au wale walao nyama kwa pupa,

21 kwa maana walevi na walafi huwa maskini,

nako kusinzia huwavika matambara.

22 Msikilize baba yako, aliyekuzaa,

wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.

23 Nunua kweli wala usiiuze,

pata hekima, adabu na ufahamu.

24 Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,

naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.

25 Baba yako na mama yako na wafurahi,

mama aliyekuzaa na ashangilie!

26 Mwanangu, nipe moyo wako,

macho yako na yafuate njia zangu,

27 kwa maana kahaba ni shimo refu

na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.

28 Kama mnyang’anyi, hungojea akivizia,

naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.

29 Ni nani mwenye ole?

Ni nani mwenye huzuni?

Ni nani mwenye ugomvi?

Ni nani mwenye malalamiko?

Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu?

Ni nani mwenye macho mekundu?

30 Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo,

hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.

31 Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu,

wakati unapometameta kwenye bilauri,

wakati ushukapo taratibu!

32 Mwisho huuma kama nyoka

na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.

33 Macho yako yataona mambo mageni

na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.

34 Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari,

alalaye juu ya kamba ya merikebu.

35 Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia!

Wamenichapa, lakini sisikii!

Nitaamka lini

ili nikanywe tena?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/23-0898d8042d66cab56ecc9751e2ae6a5b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × 1 =