Mithali 25

Mithali Zaidi Za Solomoni

1 Hizi ni mithali zaidi za Solomoni, zilizonakiliwa na watu wa Hezekia mfalme wa Yuda:

2 Ni Utukufu wa Mungu kuficha jambo,

bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo.

3 Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini,

ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki.

4 Ondoa takataka kwenye madini ya fedha,

nako ndani yake kutatokea kitu halisi

kwa ajili ya mfua fedha.

5 Ondoa waovu mbele ya mfalme,

nacho kiti chake cha enzi

kitaimarishwa kwa njia ya haki.

6 Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme,

wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu.

7 Ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,”

kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu.

Kile ulichokiona kwa macho yako

8 usiharakishe kukipeleka mahakamani,

maana utafanya nini mwishoni

kama jirani yako atakuaibisha?

9 Kama ukifanya shauri na jirani yako,

usisaliti siri ya mtu mwingine,

10 ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha

na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka.

11 Neno lisemwalo kwa wakati ufaao

ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu

yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha.

12 Kama vile kipuli cha dhahabu

au pambo la dhahabu safi,

ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima

kwa sikio lisikilizalo.

13 Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno

ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao,

huburudisha roho za bwana zake.

14 Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua

ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi.

15 Kwa njia ya uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa,

nao ulimi laini waweza kuvunja mfupa.

16 Kama ukikuta asali, kula kiasi tu cha kukutosha,

ukila zaidi, utatapika.

17 Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache,

ukizidisha, atakukinai na atakuchukia.

18 Kama vile rungu au upanga au mshale mkali

ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake.

19 Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa,

ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida.

20 Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi,

au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi,

ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito.

21 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale,

kama ana kiu, mpe maji anywe.

22 Kwa kufanya hivi, unampalia makaa ya moto kichwani pake,

nayeBwanaatakupa thawabu.

23 Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua,

ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira.

24 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba,

kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi.

25 Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka

ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.

26 Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au

kisima kilichotiwa taka

ndivyo alivyo mtu mwenye haki

anayeshindwa na uovu.

27 Si vyema kula asali nyingi sana,

wala si heshima

kujitafutia heshima yako mwenyewe.

28 Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka

ndivyo alivyo mtu

ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/25-8d43f51a751bb756c7c7ecb464c68b40.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × five =