Mithali 26

1 Kama theluji wakati wa kiangazi au mvua wakati wa mavuno,

ndivyo asivyostahili heshima mpumbavu.

2 Kama shomoro apigapigavyo mbawa zake

au mbayuwayu katika kuruka kwake kasi,

ndivyo ilivyo laana isiyo na sababu haimpati mtu.

3 Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda,

nayo fimbo kwa migongo ya wapumbavu!

4 Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,

ama wewe mwenyewe utakuwa kama yeye.

5 Mjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,

ama atakuwa mwenye hekima machoni pake mwenyewe.

6 Kama vile ilivyo kujikata miguu au kujitafutia shida,

ndivyo ilivyo kutuma ujumbe kwa mkono wa mpumbavu.

7 Kama miguu ya kiwete inavyoning’inia

ndivyo ilivyo mithali katika kinywa cha mpumbavu.

8 Kama kufunga jiwe kwenye kombeo,

ndivyo ilivyo kumpa mpumbavu heshima.

9 Kama mwiba kwenye mkono wa mlevi

ndivyo ilivyo mithali kinywani mwa mpumbavu.

10 Kama mpiga upinde ambaye hujeruhi ovyo,

ndivyo alivyo yeye aajiriye mpumbavu au ye yote apitaye njiani.

11 Kama mbwa ayarudiavyo matapishi yake,

ndivyo mpumbavu arudiavyo upumbavu wake.

12 Je, unamwona mtu ajionaye mwenye hekima

machoni pake mwenyewe?

Liko tumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko kwake.

13 Mvivu husema, “Yuko simba barabarani,

simba mkali anazunguka mitaa!”

14 Kama vile mlango ugeukavyo kwenye bawaba zake,

ndivyo mvivu ajigeuzavyo kitandani mwake.

15 Mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

naye hushindwa kuurudisha tena kinywani mwake.

16 Mvivu ni mwenye hekima machoni pake mwenyewe,

kuliko watu saba wawezao kujibu kwa busara.

17 Kama yeye amkamataye mbwa masikio,

ndivyo alivyo mtu apitaye njiani na kujiingiza kwenye ugomvi usiomhusu.

18 Kama mtu mwendawazimu

atupaye vijinga vya moto au mishale ya kufisha,

19 ndivyo alivyo mtu amdanganyaye jirani yake na kusema,

“Nilikuwa nikifanya mzaha tu!”

20 Bila kuni moto huzimika,

pasipo uchongezi ugomvi humalizika.

21 Kama makaa juu ya makaa yanayowaka na kama kuni kwenye moto,

ndivyo alivyo mtu mgomvi kwa kuchochea ugomvi.

22 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu,

huingia sehemu za ndani sana za mtu.

23 Kama rangi ing’aayo iliyopakwa kwenye vyombo vya udongo

ndivyo ilivyo midomo laini pamoja na moyo mbaya.

24 Mtu mwenye nia ya kudhuru wengine hujificha kwa maneno ya midomo yake,

lakini moyoni mwake huficha udanganyifu.

25 Ingawa maneno yake huvutia, usimwamini,

kwa maana machukizo saba hujaza moyo wake.

26 Nia yake ya kudhuru wengine inaweza kufichwa na udanganyifu,

lakini uovu wake utafichuliwa kwenye kusanyiko.

27 Kama mtu akichimba shimo, atatumbukia ndani yake,

kama mtu akivingirisha jiwe, litamrudia.

28 Ulimi wa uongo, huwachukia wale unaowaumiza,

nacho kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/26-7ddee7da96e3fbf1331eb895a9ff5efa.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

18 − 9 =