Mithali 28

1 Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna ye yote anayemfukuza,

bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

2 Wakati nchi inapokuwa na uasi, inakuwa na viongozi wengi,

bali mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utaratibu.

3 Mtu maskini amwoneaye yeye aliye maskini zaidi

ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza mazao.

4 Wale waiachao sheria huwasifu waovu,

bali wale waishikao sheria huwapinga.

5 Watu wabaya hawaelewi haki,

bali wale wamtafutaoBwanawanaielewa kikamilifu.

6 Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama

kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.

7 Yeye ashikaye sheria ni mwana mwenye hekima,

bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.

8 Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno

hukusanya kwa ajili ya mwingine,

ambaye atamhurumia maskini.

9 Kama mtu ye yote akikataa kusikia sheria,

hata maombi yake ni chukizo.

10 Yeye ambaye humwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya,

ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe,

bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.

11 Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe,

bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua.

12 Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa,

bali mwovu atawalapo, watu hujificha.

13 Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,

bali ye yote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.

14 Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humchaBwana,

bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu

huangukia kwenye taabu.

15 Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye,

divyo alivyo mtu mwovu atawalaye wanyonge.

16 Mtawala dhalimu hana akili,

bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu

atafurahia maisha marefu.

17 Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua

atakuwa mtoro mpaka kufa;

mtu ye yote na asimsaidie.

18 Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama

hulindwa salama,

bali yeye ambaye njia zake ni potovu

ataanguka ghafula.

19 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,

bali afuataye mambo ya upuzi

atakuwa na umaskini wa kumtosha.

20 Mtu mwaminifu atabarikiwa sana,

bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka

hataacha kuadhibiwa.

21 Kuonyesha upendeleo si vizuri,

hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.

22 Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri,

naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.

23 Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi,

kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.

24 Yeye amwibiaye babaye au mamaye

na kusema, “Si kosa,”

yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.

25 Mtu mwenye tamaa huchochea fitina,

bali yule amtegemeayeBwanaatafanikiwa.

26 Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu,

bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.

27 Yeye ampaye maskini

hatapungukiwa na kitu cho chote,

bali yeye awafumbiaye maskini macho

hupata laana nyingi.

28 Wakati mwovu atawalapo,

watu huenda mafichoni,

bali mwovu anapoangamia,

wenye haki hufanikiwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/28-c9b27f4f9e96255ef117c7d4b8b3ea4d.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

15 − 2 =