Mithali 27

1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,

kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.

2 Mwache mwingine akusifu,

wala si kinywa chako mwenyewe;

mtu mwingine afanye hivyo

na si midomo yako mwenyewe.

3 Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo,

lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito

zaidi kuliko hivyo vyote viwili.

4 Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika,

lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?

5 Afadhali karipio la wazi

kuliko upendo uliofichika.

6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu,

bali busu la adui ni udanganyifu.

7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,

bali kwa mwenye njaa

hata kile kilicho kichungu

kwake ni kitamu.

8 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,

ndivyo alivyo mtu atangatangaye

mbali na nyumbani mwake.

9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,

nao uzuri wa rafiki huchipuka

kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.

10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,

tena usiende nyumbani mwa ndugu yako

wakati umepatwa na maafa.

Bora jirani wa karibu

kuliko ndugu aliye mbali.

11 Mwanangu, uwe na hekima,

nawe ulete furaha moyoni mwangu,

ndipo nitakapoweza kumjibu ye yote

anitendaye kwa dharau.

12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,

bali mjinga huendelea mbele nayo ikamtesa.

13 Chukua vazi la yule awekaye dhamana

kwa ajili ya mgeni;

lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo

kwa ajili ya mwanamke mgeni.

14 Kama mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu

asubuhi na mapema,

itahesabiwa kama ni laana.

15 Mke mgomvi ni kama

matone yasiyokoma ya siku ya mvua.

16 Kumzuia yeye ni kama kuuzuia upepo

au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.

17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,

ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.

18 Yeye atunzaye mtini atakula tunda lake,

naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.

19 Kama uso uonekanavyo kwenye maji,

ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonyesha alivyo.

20 Kuzimu na uharibifu havishibi

kadhalika macho ya mwanadamu.

21 Kalibu ni kwa ajili ya fedha

na tanuru kwa ajili ya dhahabu,

bali mtu hupimwa kwa sifa azipokeazo.

22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu,

ukimtwanga kama nafaka kwa mchi,

hutauondoa upumbavu wake.

23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako

ya kondoo na mbuzi,

angalia kwa bidii ng’ombe zako.

24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,

nayo taji haidumu vizazi vyote.

25 Wakati majani makavu yameondolewa

na mapya yamechipua,

nayo majani toka milimani yamekusanywa,

26 wana-kondoo watakupatia mavazi

na mbuzi thamani ya shamba.

27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi

kukulisha wewe na jamaa yako,

na kuwalisha watumishi wako wa kike.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/PRO/27-52269f3e7dd2363a0399a4e52e2375de.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four + 3 =