Nahumu 2

Ninawi Kuanguka

1 Mshambuliaji anasogea dhidi yako, Ninawi.

Linda ngome,

chunga barabara,

jitieni nguvu wenyewe,

kusanya nguvu zako zote!

2 Bwanaatarudisha fahari ya Yakobo,

kama fahari ya Israeli,

ingawa waangamizi wamewaacha ukiwa

na wameharibu mizabibu yao.

3 Ngao za askari wake ni nyekundu,

mashujaa wamevaa nguo nyekundu.

Chuma kwenye magari ya vita chametameta,

katika siku aliyoyaweka tayari,

mikuki ya mierezi inametameta.

4 Magari ya vita yanafanya msukosuko barabarani,

yakikimbia nyuma na mbele uwanjani.

Yanaonekana kama mienge ya moto;

yanakwenda kasi kama umeme.

5 Anaita vikosi vilivyochaguliwa,

lakini bado wanajikwaa njiani.

Wanakimbilia haraka kwenye ukuta wa mji,

ile ngao ya kuwakinga imetayarishwa.

6 Malango ya mto yamefunguliwa wazi,

na jumba la kifalme limeanguka.

7 Imeagizwa kwamba mji uchukuliwe

na upelekwe uhamishoni.

Vijakazi wake wanaomboleza kama hua

na kupigapiga vifua vyao.

8 Ninawi ni kama dimbwi,

nayo maji yake yanakauka.

Wanalia, “Simama! Simama!”

Lakini hakuna anayegeuka nyuma.

9 Chukueni nyara za fedha!

Chukueni nyara za dhahabu!

Wingi wake hauna mwisho,

utajiri kutoka hazina zake zote!

10 Ameharibiwa, ametekwa nyara, ameachwa uchi!

Mioyo inayeyuka, magoti yanalegea,

miili inatetemeka,

na kila uso umebadilika rangi.

11 Liko wapi sasa pango la simba,

mahali ambapo waliwalisha watoto wao,

ambapo simba dume na simba jike walikwenda

na ambapo wana simba walikwenda

bila kuogopa cho chote?

12 Simba aliua mawindo ya kutosha watoto wake,

alinyonga mawindo kwa ajili ya mwenzi wake,

akijaza makao yake kwa alivyoua

na mapango yake kwa mawindo.

13 BwanaMwenye Nguvu Zote anatangaza,

“Mimi ni kinyume na ninyi.

Magari yenu ya vita nitayateketeza kwa moto,

na upanga utakula wana simba wako.

Sitawaachia mawindo juu ya nchi.

Sauti za wajumbe wako

hazitasikika tena.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NAM/2-a38be8b5316b20df831b93932f1e5efe.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

fourteen + 18 =