Nehemiah 13

Nehemia Afanya Matengenezo Ya Mwisho

1 Katika siku hiyo kitabu cha Mose kilisomwa kwa sauti kuu na watu wote wakasikia. Humo ilionekana imeandikwa kwamba hakuna Mwamori wala Mmoabi atakayeruhusiwa katika kusanyiko la watu wa Mungu,

2 kwa sababu hawakuwalaki Waisraeli kwa chakula na maji, badala yake walimwajiri Balaamu kuwalaani (lakini hata hivyo Mungu wetu aligeuza laana kuwa baraka).

3 Watu waliposikia sheria hii, waliwatenga watu wote wasio Waisraeli waliokuwa wa uzao wa kigeni.

4 Kabla ya hili, kuhani Eliyashibu alikuwa amewekwa kuwa msimamizi wa vyumba vya ghala ya nyumba ya Mungu wetu. Alikuwa na uhusiano wa karibu na Tobia,

5 naye alikuwa amempa Tobia chumba kikubwa ambacho mwanzo kilikuwa kikitumika kuweka sadaka za nafaka, uvumba na vyombo vya Hekalu, pamoja na zaka za nafaka, divai mpya na mafuta waliyoagizwa Waisraeli kwa ajili ya Walawi, waimbaji na mabawabu wa Lango, pamoja na matoleo kwa makuhani.

6 Lakini wakati haya yote yalipokuwa yakitendeka, sikuwa Yerusalemu, kwa kuwa katika mwaka wa thelathini na mbili wa kutawala Artashasta mfalme wa Babeli nilikuwa nimerudi kwa mfalme. Baadaye nilimwomba ruhusa,

7 nirudi Yerusalemu. Hapo niligundua jambo la uovu alilofanya Eliyashibu kwa kumpa Tobia chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.

8 Nilikasirika sana na nilivitupa nje vyombo vyote vya Tobia.

9 Nilitoa amri kutakasa vyumba, kisha nilivirudisha vifaa vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za nafaka na uvumba.

10 Pia niligundua kuwa mafungu yaliyopangwa kupewa Walawi hawakuwa wamepewa, pia Walawi wote na waimbaji waliowajibika kwa huduma walikuwa wamerudi katika mashamba yao.

11 Basi niliwakemea maafisa na kuwauliza, “Kwa nini nyumba ya Mungu imepuuzwa?” Kisha niliwaita pamoja na kuwaweka kwenye nafasi zao.

12 Yuda wote walileta zaka za nafaka, divai mpya na mafuta kwenye ghala.

13 Nikamweka kuhani Shelemia, mwandishi Sadoki na Mlawi aliyeitwa Pedaya kuwa wasimamizi wa ghala na kumfanya Hanani mwana wa Zakuri, mwana wa Matania, kuwa msaidizi wao, kwa sababu watu hawa walionekana kuwa waaminifu. Walipewa wajibu wa kugawa mahitaji kwa ndugu zao.

14 Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa hili, wala usifute kile nilichokifanya kwa uaminifu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu na kwa ajili ya huduma yake.

15 Siku hizo nikaona watu katika Yuda wakikanyaga mashinikizo ya divai siku ya Sabato na kuleta nafaka wakiwapakiza punda, pamoja na divai, zabibu, tini na aina nyingine za mizigo. Nao walikuwa wakileta haya yote Yerusalemu siku ya Sabato. Kwa hiyo niliwaonya dhidi ya kuuza vyakula siku hiyo.

16 Watu kutoka Tiro waliokuwa wakiishi Yerusalemu walileta samaki na aina nyingi za bidhaa na kuziuza Yerusalemu siku ya Sabato kwa watu wa Yuda.

17 Niliwakemea wakuu wa Yuda na kuwaambia, “Ni uovu gani huu mnaofanya kuinajisi siku ya Sabato?

18 Je, baba zenu hawakufanya mambo ya jinsi hii hata kumsababisha Mungu wetu kuleta maafa haya yote juu yetu na juu ya mji huu? Sasa bado mnazidi kuchochea ghadhabu yake dhidi ya Israeli kwa kuinajisi Sabato.”

19 Wakati vivuli vya jioni vilipoangukia juu ya malango ya Yerusalemu kabla ya Sabato, niliamuru milango ifungwe na isifunguliwe mpaka Sabato iishe. Nikawaweka baadhi ya watu wangu mwenyewe kwenye malango ili kwamba pasiwepo mzigo utakaoingizwa ndani siku ya Sabato.

20 Mara moja au mbili wachuuzi na wauzaji wa bidhaa za aina zote walilala usiku nje ya mji wa Yerusalemu.

21 Lakini niliwaonya na kuwaambia, “Kwa nini mnalala karibu na ukuta? Kama mkifanya hivi tena, nitawaadhibu.” Kuanzia wakati ule hawakuja tena siku ya Sabato.

22 Kisha nikawaamuru Walawi kujitakasa na kwenda kulinda malango ili kutunza Sabato iwe takatifu.

Ee Mungu wangu, unikumbuke kwa ajili ya hili pia, nawe unionyeshe wema wako sawasawa na upendo wako mkuu.

23 Zaidi ya hayo, niliona watu wa Yuda waliokuwa wameoa wanawake kutoka Ashdodi, Amoni na Moabu.

24 Nusu ya watoto wao walizungumza lugha ya Kiashidodi au lugha ya watu wengine, hawakuweza kuzungumza Kiyahudi.

25 Niliwakemea na kuwalaani. Niliwapiga baadhi ya watu na kung’oa nywele zao. Niliwaapisha kwa jina la Mungu na kusema: “Msiwaoze binti zenu kwa wana wao, wala binti zao wasiolewe na wana wenu wala ninyi wenyewe.

26 Je, Solomoni hakutenda dhambi kwa sababu ya wanawake wa namna hiyo? Miongoni mwa mataifa mengi hapakuwepo mfalme kama yeye. Alipendwa na Mungu wake. Naye Mungu alimweka kuwa mfalme juu ya Israeli yote, hata hivyo wanawake wa mataifa mengine walimfanya hata yeye atende dhambi.

27 Je, tulazimike sasa kusikia kwamba ninyi pia mmefanya uovu huu mkubwa na kutokuwa waaminifu kwa Mungu wetu kwa kuoa wanawake wa kigeni?”

28 Mmoja wa wana wa Yoyada mwana wa Eliashibu Kuhani Mkuu alikuwa mkwewe Sanbalati Mhoroni. Nami nilimfukuza mbele yangu.

29 Ee Mungu wangu, uwakumbuke, kwa sababu wamenajisi ukuhani na agano la kikuhani na la Walawi.

30 Kwa hiyo niliwatakasa makuhani na Walawi kutokana na cho chote kilichokuwa cha kigeni, na kuwapa wajibu, kila mmoja katika kazi yake.

31 Pia nilihakikisha kwamba matoleo ya kuni yaliletwa kwa wakati unaopaswa na malimbuko kwa wakati wake.

Ee Mungu wangu, unikumbuke, unitendee mema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/13-64e882dd6740d1962afcb87f89876d45.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

sixteen + eighteen =