Nehemiah 3

Wajenzi Wa Ukuta

1 Eliyashibu Kuhani Mkuu na makuhani wenzake walikwenda kufanya kazi na kulijenga upya Lango la Kondoo. Waliliweka wakfu na kuweka milango mahali pake, wakajenga hadi kufikia Mnara wa Mia Moja, ambao waliuweka wakfu hadi Mnara wa Hananeli.

2 Watu wa Yeriko wakajenga sehemu zilizopakana nao, Zahuri mwana wa Imri aliendelea kujenga karibu nao.

3 Lango la Samaki lilijengwa upya na wana wa Hasena. Wakaweka boriti zake, wakaweka milango yake na makomeo na nondo.

4 Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu iliyofuatia. Aliyemfuatia ni Meshulamu mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli, alifanya ukarabati na aliyemfuatia ni Zadoki mwana wa Baana.

5 Sehemu iliyofuatia ilikarabatiwa na watu kutoka Tekoa, lakini wakuu wao walikataa kufanya kazi chini ya wasimamizi wao.

6 Lango la Yeshana lilikarabatiwa na Yoyada mwana wa Pasea na Meshulamu mwana wa Besodeya. Wakaziweka boriti zake, milango, makomeo na nondo.

7 Karibu nao ukarabati ulifanywa na watu kutoka Gibeoni na Mispa, Melati ya Gibeoni na Yadoni ya Meronothi, sehemu hizi zilikuwa chini ya mamlaka ya mtawala wa Ng’ambo ya Eufrati.

8 Uzieli mwana wa Harhaya, mmoja wa masonara, walikarabati sehemu iliyofuatia na Hanania mmoja wa watengenezaji marashi, alikarabati sehemu iliyofuatia. Walitengeneza Yerusalemu mpaka kufikia Ukuta Mpana.

9 Refaya mwana wa Huri, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia.

10 Kupakana na sehemu hii, Yedaya mwana wa Harumafu alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba yake, naye Hatushi mwana wa Hashabnea alifanya ukarabati sehemu iliyofuatia.

11 Malkiya mwana wa Harimu na Hashubu mwana wa Pahath-Moabu walikarabati sehemu nyingine pamoja na Mnara wa Matanuru.

12 Shalumu mwana wa Haloheshi, mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, alikarabati sehemu iliyofuatia akisaidiana na binti zake.

13 Lango la Bondeni lilikarabatiwa na Hanuni na wakazi wa Zanoa. Walilijenga kwa upya na kuweka milango yake na makomeo na nondo mahali pake. Pia walikarabati ukuta wenye urefu wa mita 450 hadi Lango la Samadi.

14 Lango la Samadi lilikarabatiwa na Malkiya mwana wa Rekabu, mtawala wa wilaya ya Beth-Hakeremu. Alijenga kwa upya na kuweka milango yake makomeo na nondo.

15 Lango la Chemchemi lilikarabatiwa na Shalumu mwana wa Kolhoze, mtawala wa wilaya ya Mispa. Alilijenga kwa upya, akaliezeka na kuweka milango yake, makomeo yake na nondo mahali pake. Pia alikarabati ukuta wa Bwawa la Siloamu karibu na Bustani ya Mfalme hadi kwenye ngazi zinazoshuka kutoka Mji wa Daudi.

16 Sehemu iliyofuatia, Nehemia mwana wa Azbuki, mtawala wa nusu ya wilaya ya Beth-Zuri, alikarabati kufikia mkabala na makaburi ya Daudi, mpaka kwenye bwawa lililotengenezwa na kufikia Nyumba ya Mashujaa.

17 Sehemu iliofuatia, ukarabati ulifanywa na Walawi chini ya uongozi wa Rehumu mwana wa Bani. Aliyefuatia ni Hashabia, mtawala wa nusu ya wilaya ya Keila. Aliendeleza ukarabati katika sehemu inayohusu wilaya yake.

18 Sehemu iliofuatia, ukarabati ulifanywa na ndugu zao chini ya usimamizi wa Binui, mwana wa Henadadi, mtawala wa nusu ya wilaya ya Keila.

19 Sehemu iliofuatia, Ezeri mwana wa Yeshua, mtawala wa Mispa, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia ile sehemu inayotazamana na mwinuko wa kuelekea kwenye ghala la kuhifadhia silaha, mpaka kwenye pembe ya ukuta.

20 Sehemu iliofuatia, Baruki mwana wa Zabai alikarabati kwa bidii sehemu nyingine kuanzia ile pembe mpaka kwenye lango la nyumba ya Eliyashibu Kuhani Mkuu.

21 Sehemu iliofuatia, Meremothi mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, alikarabati sehemu nyingine, kuanzia penye lango la nyumba ya Eliyashibu mpaka mwisho wake.

22 Sehemu iliofuatia, ukarabati ulifanywa na makuhani kuanzia eneo lililouzunguka mji.

23 Baada yao Benyamini na Hashubu walikarabati mbele ya nyumba zao, baada yao Azaria mwana wa Maaseya, mwana wa Anania alifanya ukarabati kando ya nyumba yake.

24 Sehemu iliofuatia, Binui mwana wa Henadadi alikarabati sehemu nyingine, kuanzia kwenye nyumba ya Azaria mpaka kwenye pembe ya ukuta.

25 Naye Palali, mwana wa Uzai alijenga sehemu iliyokuwa mkabala na pembe ya ukuta mpaka kwenye mnara wa juu ambao unajitokeza kuanzia kwenye jumba la kifalme kando ya ua wa walinzi. Sehemu iliofuatia, Pedaya mwana wa Paroshi,

26 na watumishi wa Hekalu waishio juu ya kilima cha Ofeli walikarabati hadi kufikia mkabala na Lango la Maji, kuelekea mashariki pamoja na ule mnara uliojitokeza.

27 Sehemu iliofuatia, watu wa Tekoa walikarabati sehemu nyingine, kuanzia mnara mkubwa utokezao hadi ukuta wa Ofeli.

28 Makuhani walifanya ukarabati juu ya Lango la Farasi, kila mmoja mbele ya nyumba yake.

29 Baada yao, Sadoki mwana wa Imeri alifanya ukarabati mkabala na nyumba yake. Sehemu iliofuatia, Shemaya mwana wa Shekania, mlinzi wa Lango la Mashariki, alifanya ukarabati.

30 Sehemu iliofuatia, Hanania mwana wa Shelemia na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, alikarabati sehemu nyingine. Baada yao, Meshulamu mwana wa Berekia alikarabati sehemu iliyokuwa mkabala na nyumba zake za kuishi.

31 Sehemu iliofuatia, Malkiya, mmoja wa masonara, alifanya ukarabati mpaka kwenye nyumba za Wanethinina wafanyabiashara, mkabala na Lango la Ukaguzi, hadi kufikia chumba kilicho juu ya pembe.

32 Masonara na wafanya biashara walifanya ukarabati kati ya chumba kilichoko juu ya pembe ya Lango la Kondoo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/3-c90da1fa759d50072b52abd4d1b07c2f.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

17 − 13 =